Michezo

Eberechi Eze atambisha Palace dhidi ya Leeds United katika EPL

November 8th, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

EBERECHI Eze alifunga bao lake la kwanza akivalia jezi za Crystal Palace na kuongoza kikosi hicho cha kocha Roy Hodgson kupokeza limbukeni Leeds United kichapo cha 4-1 katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Novemba 7, 2020, ugani Selhurst Park.

Scott Dann alifunga kwa kicha krosi aliyopokezwa na Eze katika dakika ya 12 kabla ya Eze, 22, kupachika wavuni goli la pili kwa upande wa Palace katika dakika ya 22.

Nyota huyo aliyesajiliwa na Palace kutoka Queens Park Rangers (QPR) kwa Sh2.7 bilioni msimu huu, alichangia pia bao la tatu lililofungwa na waajiri wake kupitia kwa Jordan Ayew baada ya Helder Costa kujifunga.

Leeds ya kocha Marcelo Bielsa walifutiwa machozi na fowadi Patrick Bamford katika dakika ya 27. Ushindi wa Palace uliwapaisha hadi nafasi ya saba kwenye msimamo wa jedwali kwa alama 13 sawa na Everton waliopokezwa kichapo cha 3-1 kutoka kwa Manchester United. Leeds walishuka hadi nafasi ya 15 kwa alama 10 sawa na Man-United.

Palace waliingia ugani kwa minajili ya mechi dhidi ya Leeds wakitawaliwa na kiu ya kujinyanyua baada ya chombo chao kuzamishwa na Wolves kwa mabao 2-0 katika mchuano wa awali.

Kinyume na msimu jana ambapo walipigwa katika mechi tano kati ya saba za kwanza, Palace kwa sasa wamepoteza mechi moja pekee ligini kati ya tano zilizopita.

Ilikuwa mara ya kwanza tangu Mei 2019 walipopiga Bournemouth 5-3 kwa Palace kufunga mabao manne katika mchuano mmoja wa EPL.

Kufikia sasa, Leeds wamefungwa jumla ya mabao 17 kutokana na mechi nane za EPL. Mara yao ya mwisho kufungwa idadi hiyo ya mechi katika hatua kama hii kwenye kampeni za kipute cha EPL ni mnamo 1946-47.

Aidha, Leeds wamesajili ushindi mara moja pekee kutokana na mechi 21 zilizopita dhidi ya wapinzani wa London kwenye soka ya EPL. Walivuna ushindi wa mwisho mnamo Disemba 2017 dhidi ya QPR.

Baada ya soka ya EPL kupisha mechi za kimataifa, Palace watarejelea kampeni za msimu huu wa 2020-21 dhidi ya Burnley mnamo Novemba 21 uwanjani Turf Moor huku Leeds wakiwaalika Arsenal ugani Elland Road.