Ebola: Hofu raia wa Kenya akishukiwa

Ebola: Hofu raia wa Kenya akishukiwa

SHABAN MAKOKHA Na WINNIE ATIENO

MAAFISA wa afya nchini wameimarisha tahadhari baada ya kisa kilichoshukiwa kuwa cha ugonjwa hatari wa ebola kuripotiwa katika Kaunti ya Kakamega.

Hii ni baada ya mgonjwa mmoja, aliyekuwa amesafiri hadi Uganda, kuonyesha dalili ambazo zinahusishwa na ugonjwa huo hatari.

Ripoti ya maafisa hao wa afya ilionyesha Bw George Ashibo kutoka Kaunti-ndogo ya Nambale, Kaunti ya Busia, alikuwa amesafiri kutoka Uganda mnamo Septemba 15.

Mshirikishi wa Kituo cha Kupambana na Magonjwa ya Kuambukizana Mumias Magharibi, Boaz Gichana alisema Bw Ashibo, 32, alikuwa amezuru taifa hilo jirani.

“Septemba 28,2022, alianza kutoa mkojo wenye damu na akaenda hospitali ya St Mary’s Mumias ili kupokea matibabu zaidi. Katika hospitali hiyo alitengwa na usimamizi,” akasema Bw Gichana.

Kutokana na matokeo ya awali ya uchunguzi aliofanyiwa, Bw Ashibo alikuwa mchovu, na jeraha mguuni alikofanyiwa upasuaji lilikuwa likitoka damu. Pia mkojo wake bado ulikuwa na damu.

Naibu Gavana wa Kakamega, Ayub Savula aligusia suala hilo akisema maafisa wa afya walichukua sampuli za damu kutoka kwa mgonjwa huyo ili zifanyiwe uchunguzi katika Taasisi ya Utafiti wa Kimatibabu nchini humu (KEMRI).

Matokeo ya uchunguzi kamili yatatolewa baada ya saa 24 ili kubaini iwapo ni kisa cha ukweli cha ebola au ni ugonjwa mwingine.

“Tumewatuma maafisa wa afya katika mipaka ya kaunti yetu ili wale wanaoingia Kakamega kutoka Uganda waanze kupimwa. Ripoti ya kubaini iwapo mgonjwa huyo ana ebola au la itatolewa baada ya saa 24,” akasema Bw Savula.

Bw Savula aliwataka raia wasiingiwe na wasiwasi kwa kuwa kaunti hiyo inafanya juu chini kwa kuweka mikakati ya kuzuia ebola kuwafikia wakazi.

Wakati huo huo, wakazi wametaka serikali ya kaunti ifuatilie na kuwatenga watu ambao walitangamana na mgonjwa huyo anayeshukiwa kuwa na ebola.

Bw Kennedy Echesa alisema kuwa kati ya Septemba 15 na Septemba 30 jana, ambao mgonjwa huyo alisafiri Uganda na kurejea, alitangamana na watu wengi na hata wao wanastahili kutengwa.

Bw Echesa alilaumu serikali na wizara ya Afya kwa kulegea huku raia wakiendelea kuingia Kenya kutoka Uganda na Wakenya kuelekea huko bila kupimwa mpakani.

Nao maafisa wa afya katika bandari ya Mombasa na uwanja wa kimataifa wa ndege wa Moi wameimarisha usalama katika maeneo hayo wakihofia mlipuko wa ebola inayoendelea kuenea kwa kasi nchini Uganda.

Aidha, wizara ya Afya ilitaja Mombasa kuwa kati ya kaunti 20 ambazo ziko katika hatari kufuatia shughuli za uchukuzi wa bidhaa kati ya Kenya na Uganda.

Maafisa wa afya wameanza kukagua wageni wanaowasili nchini kupitia uwanja huo wa ndege.

Afisa wa Afya ya Umma, Kaunti ya Mombasa, Bi Pauline Oginga alisema serikali hiyo ya ugatuzi imeimarisha ukaguzi na kuweka mikakati kabambe ya kuepuka mlipuko na maambukizi ikiwemo kufungua kituo maalum cha washukiwa wa ebola katika kituo cha afya cha Railways.

  • Tags

You can share this post!

Kocha Jurgen Klopp atetea beki Alexander-Arnold baada ya...

Gavana Nassir kuimarisha idara kukabili majanga

T L