Ebola: Idadi ya vifo yaongezeka Uganda

Ebola: Idadi ya vifo yaongezeka Uganda

NA DAILY MONITOR

KAMPALA, UGANDA

SERIKALI ya Uganda imesema kuwa visa vya maradhi hatari ya Ebola vimesambaa katika maeneo zaidi nchini humo, huku ikiwatahadharisha raia kuchukua tahadhari za kujikinga.

Idadi ya watu waliofariki pia imeongezeka na kufikia 19, kulingana na taarifa iliyotolewa na Wizara ya Afya nchini humo hapo jana Jumapili.

Wizara hiyo ilisema kuwa visa zaidi vimethibitishwa katika wilaya za Kampala, Kisoro, Kakumiro, Mubende na Kyegewa.

Kando na kujilinda dhidi ya kuambukizwa, idara za afya zimewashauri raia kuripoti kuhusu watu wanaoonekana kuwa na dalili za maradhi hayo.

Wizara ilieleza kuwa tayari, sampuli za watu wanaoshukiwa kuwa na maradhi hayo zimepelekwa katika Taasisi ya Kuchunguza Virusi ya Uganda (UVRI) ili kufanyiwa utafiti.

Wizara hiyo ilisema kuwa kufikia Jumamosi, watu 31 walikuwa wamethibitishwa kuambukizwa.

Hilo ni ikilinganishwa na visa saba pekee vilivyokuwa vimethibitishwa Jumanne wiki iliyopita, maradhi hayo yalipothibitishwa.

Msimamizi Mkuu wa mipango ya kudhibiti maradhi hayo, Dkt Henry Kyobe, alisema kuwa visa vingi vipo katika wilaya ya Mubende, iliyo kitovu kikuu cha maradhi hayo.

Kaunti ndogo za Madudu, Kiruuma na Kasambya pia zimeripoti visa zaidi vya maradhi hayo.

Katika wilaya ya Kyegegwa, jumla ya visa sita na kifo kimoja vimeripotiwa. Idara za afya zilisema zinafuatilia hali za watu 20 wanaotuhumiwa kutangamana na watu waliombukizwa maradhi hayo.

Katika wilaya ya Kisoro, iliyo umbali wa kilomita 413 kutoka wilaya ya Mubende, visa viwili vimeripotiwa.

Ikiwa vitathibitishwa, basi inamaanisha huenda maradhi hayo yakasambaa kwa kasi.

Wataalamu wanaeleza kusikitishwa na kifo kimoja kilichoripotiwa jijini Kampala, ikizingatiwa ikilinganishwa na maeneo mengine, ndilo lenye idadi kubwa zaidi ya watu.Msimamizi Mkuu wa huduma za afya jijini Kampala, Dkt Daniel Okello, alisema kuwa sampuli kutoka kwa mtu aliyefariki kutokana na maradhi hayo tayari zimepelekwa katika taasisi ya UVRI ili kufanyiwa uchunguzi.

Msimamizi huyo alionya kuwa huenda visa hivyo vikasambaa zaidi, ikiwa raia hawatashirikiana ifaavyo na wahudumu wa afya.Wilaya ya Mubende iko kwenye mojawapo ya barabara kuu zinazoelekea jijini Kampala kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Ina maeneo mengi ya kibiashara ambako watu hutangamana kwa wingi.

Kulingana na Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Kushughulikia Dharura kuhusu Afya ya Umma (PHEOC), Dkt Issa Makumbi, taifa hilo limechelewa kukabili msambao wa maradhi hayo kwani serikali haikuwa ikitarajia yangezuka katika wilaya ya Mubende.

Alisema vituo vya afya vya kibinafsi havikuwa vikichukulia maradhi hayo kwa uzito, hadi pale yalitangazwa kusambaa katika maeneo kadhaa.

Inaripotiwa maradhi hayo yalizuka mwanzoni mwa mwezi huu wa Septemba ijapokuwa yalibainika baada ya wiki mbili, yaliposambaa na kuwaathiri makumi ya watu.

Serikali za mataifa jirani kama Kenya na Tanzania zimeanza kuwaweka raia wake katika hali ya tahadhari.

  • Tags

You can share this post!

WANDERI KAMAU: Hivi ndivyo tutakavyojiokoa kutoka katika...

Brigid Kosgei ajiondoa London Marathon kuuguza jeraha

T L