Kimataifa

Ebola yasababisha kifo cha mtoto nchini Uganda

August 30th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

UGANDA imesema kuwa imethibitisha kisa cha pili cha ugonjwa hatari wa Ebola nchini humo miezi miwili na nusu baada ya visa vitatu kuripotiwa.

Maafisa wa wizara ya afya wa Uganda walithibitisha kuwa msichana mwenye umri wa miaka tisa kutoka Jamhuri ya Demokrasia ya Congo alipatikana na ugonjwa huo katika wilaya ya Kasese.

Yusuf Baseka, afisa wa afya katika wilaya ya mpakani ya Kasese inayopatikana Magharibi mwa Uganda, ameliambia shirika moja la habari kwamba msichana huyo amefariki Ijumaa katika kituo cha afya cha Bwera ambako alikuwa akipokea matibabu.

Kwenye taarifa, wizara ilisema kuwa msichana huyo alikuwa na mama yake. Habari hizo zinajiri wakati visa 3,000 vya Ebola vimeripotiwa DRC ambapo maradhi hayo yamesababisha vifo vya watu 2006.

Kulingana na taarifa ya wizara ya afya ya Uganda, msichana huyo na mama yake walivuka mpaka eneo la Mpondwe, wilaya Kasese ambapo visa vya awali vya Ebola viliripotiwa.

Matabibu katika kituo cha Mpondwe waligundua kuwa msichana huyo alikuwa na joto jingi, alikuwa dhaifu na kutokwa na damu mdomoni na wakamtenga na watu wengine.

Wizara ya afya ilisema kwamba msichana huyo alihamishiwa hospitali ya Bwera ambayo ina kitengo cha kushughulikia Ebola.

Watu waliogunduliwa kuwa na ugonjwa huo mwezi Juni pia walitibiwa katika hospitali hiyo. Uchunguzi uliofanywa na wataalamu wa taasisi ya utafiti wa virusi ya Uganda iliyoko Entebbe ulithibitisha kuwa msichana huyo alikuwa na Ebola.

Maafisa wa wizara ya afya walisema kwamba msichana huyo hakugusana na yeyote isipokuwa mama yake tangu alipoingia Uganda.

“Wizara ya Afya inataka kusisitizia umma ushirikiane na maafisa wa afya, uhamiaji na usalama ili kuhakikisha ukaguzi umefanywa kikamilifu katika vituo vyote vya kuingia nchini ili kuzuia kuenea kwa Ebola maeneo mengine nchini,” ilisema taarifa ya wizara.

Bwera iko kilomita 472 kutoka jiji kuu la Uganda, Kampala.

Hofu

Kuripotiwa kwa kisa hicho kunaongeza hofu kwamba ugonjwa huo umeenea kutoka mikoa ya Kivu Kaskazini na Ituri nchini DRC.

Mnamo Juni 14, maafisa walithibitisha kisa kimoja cha ugonjwa huo katika jiji la Goma, makao makuu ya mkoa wa Kivu Kusini. Kisa cha pili cha Ebola kilithibitishwa katika mji huo Julai 30.

Mnamo Agosti 16 maafisa wa DRC waliripoti kuwa ugonjwa huo ulikuwa umeenea hadi mkoa wa South Kivu na eneo la mashambani la Pinga lililoko North Kivu.

Kamati ya kukabiliana na Ebola nchini DRC ilisema kati ya visa 14 vilivyoripotiwa Alhamisi, saba viligunduliwa North Kivu, tatu mjini Beni, na kimoja katika maeneo ya 1 Mutwanga, Kalunguta, Katwa, na Mabalako.

Visa vinne viliripotiwa Mambasa na mbili Mandima katika mkoa wa Ituri ilhali kisa kimoja kilipatikana Mwenga, mkoa wa Kivu Kusini.