Habari Mseto

Ebrahims yatia kikomo kwa biashara ya miaka 75

February 7th, 2019 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

Baada ya miaka 75 sokoni, duka la rejareja la Ebrahims katika Barabara ya Moi, Nairobi, limefungwa.

Duka hilo liliuza bidhaa zake kwa bei ya chini wiki jana na kumaliza mauzo hayo Jumamosi na kufunga duka hilo.

Kulingana na tangazo, jumba lililohifadhi duka hilo litageuzwa kuwa vyumba vya kutumiwa kwa biashara tofauti.

Kutokana na hatua hiyo, takriban wahudumu 30 walipoteza kazi katika duka hilo lililoanzishwa kabla ya uhuru.

Wamiliki wa duka hilo hawakujibu maswali kuhusiana na hatua hiyo. Duka la Ebrahim lilifunguliwa 1944 na kufikia sasa limefunga matawi yake Kisumu, Nakuru na Mombasa.