HabariSiasa

Echesa achunguzwe alivyoingia kwa ofisi yangu – Ruto

February 19th, 2020 3 min read

Na BENSON MATHEKA

Uchunguzi kuhusu kashfa ya utapeli inayodaiwa kuhusisha ofisi ya Naibu Rais William Ruto unapoendelea, maswali yanazidi kuibuka kuhusu iwapo Dkt Ruto binafsi alifahamu njama hiyo.

Wapelelezi waliopiga kambi katika ofisi yake kwa siku tatu kufuatia kukamatwa kwa aliyekuwa Waziri wa Michezo Rashid Echesa na washukiwa wengine watatu wamewaita maafisa wakuu katika ofisi ya Ruto kuwahoji.

Bw Echesa na wenzake walikamatwa nje ya ofisi hizo baada ya kutia sahihi kandarasi feki ya kununua silaha na wakurugenzi wa kampuni ya Eco Advanced Technology kutoka Poland.

Wapelelezi wamebaini kwamba kandarasi hiyo feki ilitiwa sahihi katika Harambee Annex, afisi rasmi ya Dkt Ruto.

Bw Echesa ni mwandani wa Dkt Ruto na kuna wanaouliza iwapo njama ya mabilioni ya pesa ingefanyika katika ofisi yake bila yeye kufahamu.

Maafisa wa upelelezi walisema kwamba washukiwa hao walipatikana na stakabadhi ghushi za kandarasi wakidai zilikuwa zimetoka wizara ya ulinzi.

Wizara hiyo imejitenga na stakabadhi hizo na kusema wakurugezi wa kampuni hiyo Stanley Kozlowski na Momdou Mostafa Amer hawakutembelea Wizara ya Ulinzi.

Kulingana na stakabadhi hizo, tenda hiyo ilikuwa ya kununua silaha za kima cha Sh39.5bilioni.

Jumatano, Dkt Ruto aliyekutana na wafanyakazi wa ofisi yake ya Harambee Annex katika afisi yake iliyoko mtaani Karen, alimwandikia barua Inspekta Jenerali wa polisi Hillary Mutyambai akimtaka achunguze jinsi wageni waliweza kuingia katika ofisi zake.

Kwenye barua yake, Dkt Ruto anasema Bw Echesa na wageni wawili waliingia katika chumba cha wageni katika orofa ya pili hatua ambayo inazua wasiwasi kuhusu usalama katika ofisi hizo.

“Tukio hili ni hitilafu kubwa kwa usalama wa Naibu Rais na linahitaji kuchunguzwa kikamilifu,” inasema barua iliyoandikwa na mkuu wa wafanyakazi katika ofisi ya Dkt Ruto, Bw Ken Osinde.

Dkt Ruto anataka maafisa wa usalama waliomruhusu Echesa na wenzake katika ofisi hizo watambuliwe.

Katika hatua inayoweza kubadilisha mkondo wa uchunguzi, Dkt Ruto anamtaka Bw Mutyambai kuwachunguza wawekezaji waliodai walitapeliwa na Echesa.

Anataka uchunguzi uelekezwe kubaini nia yao nchini, iwapo wana vibali vya kuwa nchini na kwa nini walikuwa katika ofisi yake Februari 13.

“Wizara ya mashauri ya kigeni inapaswa kutoa habari kuhusu raia hawa wawili wa kigeni na maelezo ya kampuni wanazodai wanawakilisha,” inaeleza barua hiyo. Bw Ruto anataka wawekezaji hao wazuiwe kuondoka nchini hadi uchunguzi anaotaka ukamilike.

Aidha, anataka kampuni ya Eco advance Technology ichunguzwe kubaini iwapo ina wawakilishi humu nchini na aina ya biashara inayofanya.

Haya yanajiri baada ya wapelelezi kutambua wafanyakazi saba kutoka afisi ya Harambee Annex ambao itahoji kuhusu sakata hiyo. Wapelelezi wanakagua kamera za usalama baada ya kupata vidokezo kwamba Bw Echesa na wenzake walikutana katika ofisi hiyo Januari 20 mwaka huu kupanga utapeli huo.

Duru zinasema kuwa wapelelezi wanapekua kompyuta za baadhi ya wafanyakazi ili kubaini iwapo kuna yeyote aliyewasiliana kwa barua pepe na kampuni ya Eco Advanced Technologies.

Bw Kozlowski aliambia wapelelezi kwamba alipokea barua pepe ikimjulisha kuhusu zabuni ya kununua vifaa vya kijeshi katika wizara ya ulinzi.

Simu za washukiwa pia zinakaguliwa ili kubaini ni nani waliyewasiliana nao kabla ya kuwapeleka wakurugenzi wa kampuni hiyo katika afisi ya Dkt Ruto.

Inasemekana kuwa huenda mkutano mmoja wa kupanga njama hizo ulifanyika nchini Sudan Januari 14 mwaka huu.

Wakati huo, Dkt Ruto alizuru nchini humo katika ziara ya siri ambayo baadaye alieleza kwamba alitembelea mradi wa kufunga kuku wa mayai.

Duru zilisema kwamba wapelelezi wa kimataifa (Interpol) wameshirikishwa katika uchunguzi huo.

Baadhi ya wakosoaji wa Dkt Ruto wamemtaka ajiuzulu kuruhusu uchunguzi huru kufanyika ingawa wapelelezi wamebainisha kuwa hakukutana na Bw Echesa siku aliyokamatwa.

Mkurugenzi wa mawasiliano katika ofisi ya Dkt Ruto David Mugonyi alisema kupitia taarifa kwamba naibu rais hakukanyaga ofisi yake ya Harambee Annexe siku hiyo wala hakuwa amepanga kukutana na Bw Echesa.

Duru zinasema kuwa wapelelezi wanakagua simu za washukiwa ili kubaini maeneo waliyokutania na kuwatambua washukiwa wengine saba akiwemo mwanasiasa mwanamke kutoka eneo la Kati ambaye inaaminika aliwashawishi wakurugenzi wa kampuni ya EAT kumuamini Bw Echesa.

Mnamo Jumanne jioni, mpokeaji wageni katika ofisi ya Dkt Ruto aliandikisha taarifa katika ofisi za DCI.

“Kundi jingine linatarajiwa kuhojiwa kuanzia Jumatano na kuendelea. Tunataka kumakinika kabisa,” alisema afisa anayehusika na uchunguzi huo.

Wapelelezi wanakagua kamera za usalama katika hoteli ya Hemingways iliyoko Karen, jumba la mikutano la KICC ambako inasemekana Echesa aliwapeleka wakurugenzi hao kukutana na mwanasiasa fulani, na katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta International Airport (JKIA) ambako washukiwa na wawekezaji yao inasemekana walikutana.

Haya yanajiri huku uraia wa Kozlowski ukiibua maswali baada ya kuibuka kuwa alisajili kampuni yake nchini kama Mkenya.

Rekodi katika ofisi za msajili wa kampuni zinaonyesha kuwa kampuni kwa jina Eco Advanced Technology ilisajiwa Desemba 5 2016, Stanley Kozlowski, raia wa Kenya, akiwa mmoja wa wamiliki wake.

Mnamo Alhamisi wiki jana, aliambia wapelelezi kwamba yeye ni raia wa Amerika aliyewekeza Poland ambako kampuni yake inapatikana.