Habari Mseto

Echesa alakiwa kishujaa licha ya kesi kortini

October 24th, 2020 1 min read

Na SHABAAN MAKOKHA

ALIYEKUWA Waziri wa Michezo Rashid Echesa, Ijumaa alikaribishwa kishujaa mjini Mumias akirejea nyumbani kwa mara ya kwanza baada ya mwaka mmoja.

Bw Echesa hajawahi kufika Mumias tangu kesi iliyomhusisha na sakata ya Sh39 bilioni za kununua bunduki feki mapema mwaka 2020.

Ijumaa, shughuli za kibiashara katika mji wa Mumias zilisimama kwa muda baada ya mamia ya wafuasi wa Bw Echesa kujazana mjini humo kumkaribisha mwana wao nyumbani.

Msafara wake ulipitia kituo cha kibiashara cha Ekero hadi mjini Mumias kisha wakamsindikiza hadi nyumbani kwake Shibale huku wakiimba nyimbo za kishujaa za Kiluhya. Walidai kwamba mwanao alikwamishwa jijini Nairobi kutokana na ‘nguvu za giza’.

Bw Echesa naye alisimama kwenye gari moja lililokuwa katika msafara huo huku akiwapungia mkono. Alisimama katika soko la Sabatia mjini Butere kuwahutubia wafuasi wake ambao waliziba barabara wakitaka kusikia kutoka kwake.