Habari MsetoSiasa

Echesa alivyojifanya msaidizi wa Ruto

February 17th, 2020 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

ALIYEKUWA waziri wa michezo Rashid Echesa alimtia Naibu Rais William Ruto taabani alipojitambulisha kwa wawekezaji wawili wa kimataifa kuwa msaidizi wake wa kibinafsi na kutia saini kandarasi za kuiuzia idara ya jeshi vifaa vya mawasiliano na ulinzi vya thamani ya Sh39.5 bilioni.

Echesa alikana mashtaka 11 mbele ya hakimu mwandamizi mahakama ya Milimani Kennedy Cheruiyot.

Echesa alikana alijitambua kuwa msaidizi wa kibinafsi wa Ruto kwa Mabw Kozlowski Stanley Bruno na Mamdough Mostafa Amer Lofty mnamo Feburuari 13 2020 katika afisi ya Ruto iliyoko Harambee House Annex jijini Nairobi.

Waziri huyo wa zamani alishtakiwa pamoja na washukiwa wengine watatu Daniel Otieno Omondi almaarufu Jenerali Juma,Clifford Okoth Onyango almaarufu Paul na Kennedy Oyoo Mboya.

Bw Omondi alijitambua kwa Mabw Bruno na Mostafa kuwa yeye ni Jenerali Juma wa Idara ya Ulinzi (DoD).

Katika afisi ya naibu wa rais wanne hao mnamo Feburuari 13 mwaka huu wakiwa na watu wengine ambao hawakufikishwa kortini walimkabidhi Mostafa mkataba uliotiwa sahini kati ya Serikali ya Kenya na Kampuni ya Eco Advanced Technologies LLC wa kuiuzia DoD vifaa vya kiusalama na mawasiliano.

Echesa, Omondi, Onyango na Mboya walikabiliwa na shtaka la pamoja la kujaribu kupokea Sh39,544,2000,000 kutoka kwa Bw Bruno wakidai atapewa kandarasi ya kuiuzia DoD vifaa vya kiusalama na mawasiliano.

Pia walikabiliwa na shtaka la kupokea kwa njia ya undanganyifu Sh11, 500, 800 kutoka kwa Bw Bruno.

Washtakiwa hao wanne walikabiliwa na shtaka la kuunda kandarasi na mikataba ya mauzo ya vifaa vya mawasiliano.

Walikanusha mashtaka walitayarisha mikataba na kampuni ya Poland. Waliwakilishwa na Cliff Ombeta na Evans Ondieki na kiongozi wa mashtaka alikuwa Jacinta Nyamosi.

Nyamosi alipinga wakiachiliwa kwa dhamana akisema watavuruga mashahidi na ushahidi.

Ombeta alieleza mahakama hakuna ushahidi kuwa washukiwa hao watavuruga mashahidi aliosema ni maafisa wa kijeshi na polisi.

Mahakama iliamuru waachiliwe kwa dhamana ya Sh1 milioni.