Habari MsetoSiasa

Echesa amtoroka Ruto, aunga Mudavadi

June 9th, 2019 2 min read

Na SHABAN MAKOKHA

ALIYEKUWA Waziri wa Michezo Rashid Echesa amegura kambi ya Naibu Rais William Ruto na kumuunga mkono kinara wa Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi kuhusiana na azma yake ya urais mwaka wa 2022.

Akizungumza jana mjini Mumias, Bw Echesa alisema kuwa kinara huyo wa ANC ana nafasi nzuri ya kupeperusha bendera ya jamii ya Waluhya katika juhudi zake za kutwaa uongozi wa taifa.

“Watu wanachukulia kwa mzaha unyenyekevu wa Mudavadi na kuipuuza jamii ya Waluhya. Lakini wajue kwamba kuna viongozi wengine katika jamii ambao wanaweza kutoa mwelekeo. Tunamtaka ndugu yetu mkubwa Mudavadi kudhihirisha ubabe wake na kutwaa uelekezi wa jamii akijua tuko nyuma yake,” alisema Bw Echesa.

Waziri huyo wa zamani alitoa tangazo hilo katika kijiji cha Mwikali, Mumias Mashariki, wakati wa mazishi ya Mama Jescah Afandi, mamaye David Wamatsi ambaye ni mwanasiasa tajika eneo la Mumias.

Bw Echesa alisema kwamba yuko tayari kujiunga na chama cha ANC iwapo Bw Mudavadi atajitokeza na kuonyesha ubabe wake wa uongozi.

Katika matamshi yaliyodhihirisha kuwa mfuasi huyo sugu wa Bw Ruto na mpinzani mkali wa Bw Mudavadi ameanza kuegemea upande wa kinara wa ANC, alisisitiza kuwa jamii ya Waluhya lazima itaunda serikali ijayo kwa kuwa na mgombea mmoja wa urais ama kuwa na wanachama katika nyadhifa za uongozi serikalini.

Alieleza: “Niko tayari kufanya chochote kuhakikisha kwamba mgombea kutoka jamii ya Waluhya anatwaa uongozi wa taifa. Lakini hilo lawezekana tu iwapo Mudavadi, ambaye ameonyesha sifa tosha za kuwa rais, ataondoka katika maeneo yake ya kawaida ili tumpigie debe kwa jamii nyingine katika harakati za kusaka uungwaji mkono wao.”

Bw Echesa alimtaka kinara huyo wa ANC kuwarai Waluhya kote kote kuungana naye ili wampe tiketi ya kuwania urais.

Alisema kwamba Waluhya wametapakaa katika vyama vingine hususan Jubilee, ODM na Ford Kenya na hilo limeathiri jaribio lao la kuwa na mgombea mmoja wa urais kutoka jamii hiyo.