Echesa anaswa akimzaba kofi afisa wa IEBC katika uchaguzi mdogo Matungu

Echesa anaswa akimzaba kofi afisa wa IEBC katika uchaguzi mdogo Matungu

Na SAMMY WAWERU

ALIYEKUWA Waziri wa Michezo Rashid Eshesa amejipata pabaya baada ya kunaswa akimzaba kofi mmoja wa afisa wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) katika mojawapo ya vituo vya kupiga kura eneobunge la Matungu, Kakamega kwenye uchaguzi mdogo uliofanyika Alhamisi.

Wapigakura eneobunge hilo walishiriki uchaguzi mdogo kuchagua mbunge wao, baada ya kiti hicho kusalia wazi kutokana na kifo cha aliyekuwa mbunge, Bw Justus Murunga (ANC) Novemba 2020.

Kwenye video inayosambaa mitandaoni, Bw Echesa anaonekana akijibizana na afisa huyo, akitaka kuelezwa sababu za maajenti wa chama cha UDA kufurushwa kituoni.

Ni malumbano yanayoishia waziri huyo wa zamani kumuangushia afisa huyo wa IEBC kofi.

Chama cha UDA kinahusishwa na Naibu wa Rais Dkt William Ruto, ambapo kina mgombea, Bw Alex Lanya ambaye ameshiriki kuwania ubunge Matungu.

“Maajenti wetu wako nje ya kituo rafiki yangu. Huwezi ukawafukuza. Kwa nini ukawatimua? Ni nani alikuagiza uwafurushe?” Bw Echesa akataka kujua.

Uchaguzi mdogo wa Matungu umetajwa kuwa kinyang’nyiro cha farasi watatu, ambapo mbali na UDA, chama cha ODM pia kimeshiriki, Bw Paul Were akipeperusha bendera, na ANC kupitia mwaniaji wake, Bw Oscar Nabulindo.

You can share this post!

Were aongoza Zesco United kutesa ligini Zambia NAPSA Stars...

Mwalimu amkata mwenzake wakipigania msichana wa chuo