Habari MsetoSiasa

Echesa asirudishiwe silaha wala gari – DPP

June 18th, 2020 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MKURUGENZI wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji alikata rufaa kupinga agizo polisi wamrudishie aliyekuwa waziri wa michezo Rashid Echesa bastola mbili na gari la thamani ya Sh23 milioni zilizotwaliwa alipokamatwa na kushtakiwa katika kashfa ya silaha ya thamani ya Sh40 bilioni.

DPP anaomba mahakama kuu ifutilie mbali agizo la hakimu mwandamizi Kennedy Cheruiyot kwamba polisi wamrudishie tena Bw Echesa silaha hizo.

Kiongozi wa mashtaka Bi Jacinta Nyamosi , amesema katika ombi alilowasilisha mbele ya Jaji Ngenye Macharia kwamba “bastola hizo na gari hilo ni miongoni mwa ushahidi utakaotolewa katika kesi hiyo ya kashfa ya silaha.”

DPP anaomba mahakama kuu ifutilie mbali agizo hilo na kuruhusu kesi iendelee ndipo ushahidi alionao uwasilishwe kortini.

Kesi hiyo haikuendelea kwa vile mtandao wa Skype ulikuwa na hitilafu. Jaji Macharia aliiahirisha hadi Juni 23.

Bw Echesa ameshtakiwa katika kashfa hiyo ya silaha iliyohusisha kampuni moja ya Amerika kwa jina Echo Advanced Technologies.

Ijapokuwa hakimu aliamuru bastola na silaha zirudishwe alikataa kuamuru akaunti za Bw Echesa zifunguliwe.

Akaunti hizo zilifungwa kufuatia ombi la Polisi baada ya wakurugenzi wa kampuni hiyo ya Amerika kulalamika walifujwa pesa.

akisema“hakukabidhiwa agizo la Mahakama kuu Kakamega iliyoamuru zifungwe.”

“Sikuona agizo iliyoamuru akaunti hizo zifungwe kwa hivyo ombi hilo halitajadiliwa,” alisema Bw Cheruiyot.

Hakimu alikubalia ombi la Bw Echesa kupitia kwa mawakili Cliff Ombeta, Bryan Khaemba na Evans Ondieki kwamba bastola hizo na gari hazina uhusiano na kashfa hiyo.

Bw Cheruiyot alisema kuwa waziri huyo wa zamani hajashtakiwa kwa kosa lolote kuhusu silaha ama kudaiwa alimnyang’anya mtu gari hilo.

“Ushahidi uliowasilishwa kortini umesema Bw Echesa aliuziwa gari hilo kwa bei ya Sh23milioni na hakuna dai lolote kuhusu gari hilo,” alisema Bw Cheruiyot.

Baada ya kusema kwamba bastola na gari hilo hazina uhusiano wowote na kesi anayoshtakiwa hakimu aliamuru arudishiwe mara moja.