Bambika

Eddie Butita: Ukitafuta mapenzi kwa familia ‘high-class’ simu yako inanuswa

January 12th, 2024 2 min read

NA MWANGI MUIRURI

MCHESHI Eddie Butita,31, ‘amewawon’ wasanii wa kiume dhidi ya kurusha mistari kwa warembo kutoka kwa familia zenye uwezo na ushawishi mkubwa.

Butita anadai kwamba kuchumbia ‘mtoto high-class’ ni sawa na kualika simu yako kunuswa mara kwa mara.

Aidha mcheshi huyo alijiunga na wengi ambao wamemtaka mwanamuziki Daddy Owen aweke wazi urafiki wake kwa binti wa Rais William Ruto, mwanadada Charlene Ruto, ni wa aina gani.

Hii ni baada ya safu za burudani kuchambua ‘utambulisho’ ambapo Charlene alikaribishwa Kakamega akamuone mamake mwanamuziki huyo maarufu.

Akitania, Butita alimuambia: “Ukioa huyo ujue ni kama jela umejiingiza kwani maisha yako yatapoteza usiri na msimamo.”

Akifahamika kwa majina kamili Edwin Butita, kando na ucheshi huwa anaigiza, na ni mwandishi, emcee na pia mwelekezi wa filamu.

Kwa pamoja yeye hujitambulisha kama mfanyabiashara wa kazi za sanaa.

“Nakuonya kwamba simu yako itakuwa inadukuliwa na jumbe zako kusomwa. Huyo yuko na vitengo vya kiusalama kama wapelelezi wa makosa ya jinai (DCI) na majasusi (NIS),” akasema.

Wadaku wa safu ya burudani waliingiwa na uvumi kwamba Owen na Charlene walikuwa na uvutio wa uchumba baada ya kutembelea wazazi wa kidume katika Kaunti ya Kakamega hivi majuzi.

Msanii Daddy Owen akiwa na Bi Charlene Ruto. PICHA | HISANI

Ngoma, semi, miondoko na utani kati yao uliwaangazia kama waliokuwa wamefika awamu ya mapenzi ambapo kama kikohozi, hayafichiki eti.

“Lakini naomba tusifike huko, sio kila mara wawili wakionekana pamoja inakuwa ni kasheshe…nimekuwa katika haya mambo ya usanii kwa miaka 20 sasa…sisi ni marafiki wa kufaana lakini hayo mengine kwa sasa tuyakome,” akasema Owen ambaye jina lake kamili ni Owen Mwaita.

Katika mitandao yake ya kijamii Owen amekuwa akishikilia kwamba uhusiano wake na Charlene ni ule wa kuwafaa waja mashinani na miradi mingine ya usanii.

Mnamo siku ya Krismasi, wawili hao walionekana katika vituo vya matatu wakitoa zawadi na tuzo nyingine haswa kwa vijana.

Hata hivyo, Butita amemshauri Owen kwamba iwapo itafika awamu ya mapenzi, achukue tahadhari kwa kuwa “hata mkikosana na Charlene, msimamo wako na maoni yako hayatakuwa na maana kwa kuwa utakuwa wa kupangwa”.

[email protected]