Michezo

Eden Hazard kula mshahara wa juu kuliko wote Real Madrid, ampiku Bale

June 8th, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE na MASHIRIKA

MCHEZAJI aliyekuwa alikilipwa mshahara wa juu kabisa katika klabu ya Chelsea, Eden Hazard sasa atavuna mshahara wa juu kabisa katika klabu yake mpya ya Real Madrid baada ya kujiunga na miamba hawa wa Uhispania kwa Sh16.7 bilioni.

Kwa mujibu wa gazeti la Evening Standard, Mbelgiji huyu, ambaye alitua Madrid kutoka Chelsea hapo Juni 7, atampiku raia wa Wales Gareth Bale.

Bale aliongoza orodha ya walaji wa mshahara mkubwa kwa kuvuna Sh44.6 milioni kila wiki ama Sh2.3 bilioni kila mwaka, baada ya Mreno Cristiano Ronaldo kuhamia Juventus.

Mjerumani Toni Kroos na nahodha Sergio Ramos wote hupokea Sh25.7 milioni kila wiki, raia wa Croatia Luka Modric analipwa Sh23.2 milioni kila wiki.

Hazard alijiunga na Real ya kocha Zinedine Zidane kwa kandarasi ya miaka mitano. Atatambulishwa kwa mashabiki wa Real hapo Juni 13. Winga huyu matata alifungia Chelsea mabao 110 katika mechi 352 tangu atue kutoka Lille nchini Ufaransa mwaka 2012.

Wachezaji wanaolipwa mshahara mkubwa Real Madrid:

Eden Hazard – Sh51.5 milioni

Gareth Bale – Sh44.6 milioni

Toni Kroos – Sh25.7 milioni

Sergio Ramos – Sh25.7 milioni

Luka Modric – Sh23.2 milioni

Karim Benzema – Sh19.3 milioni