Eid: Viongozi wavunja desturi ya Kiislamu sababu ya siasa

Eid: Viongozi wavunja desturi ya Kiislamu sababu ya siasa

VALENTINE OBARA na ABDULRAHMAN SHERIFF

ITIKADI za dini ya Kiislamu zilivunjwa Jumatano wakati wa sherehe za Eid-Ul-Adha Kaunti ya Mombasa, ili kuwezesha viongozi wa kike kuwashambulia kwa maneno mahasimu wao wa kisiasa.

Wakati wa sherehe ambayo iliandaliwa katika ukumbi wa Bhadalla, wanawake na wanaume walikuwa wametenganishwa ukumbini jinsi inavyostahili kidini.

Hata hivyo, baada ya viongozi wa kiume waliokuwa jukwaani kukamilisha hotuba zao, Gavana wa Mombasa Hassan Joho alisisitiza baadhi ya wenzao wa kike wafululize hadi jukwaani kuhutubia wageni waliohudhuria.

Kando na Bw Joho, viongozi wengine waliokuwa jukwaani ni kinara wa ODM Raila Odinga, Mbunge wa Kipipiri Amos Kimunya, Mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir miongoni mwa wengine.“Waache si wamevaa hijab wote.

Waje hapa tu shida iko wapi? Hawa ni baba zake na mama zake. Si wamevaa kiheshima wanaweza kuingia, hapa sio msikitini,” akasema gavana huyo, huku manung’uniko yakisikika miongoni mwa baadhi ya wanaume waliokuwa ukumbini.

Alikuwa akiwaita Mbunge wa Likoni Mishi Mboko, Mbunge Mwakilishi wa Wanawake Mombasa Asha Mohamed, mwenzake wa Wajir Fatuma Gedi na Waziri Msaidizi wa Utumishi wa Umma na Jinsia Rachael Shebesh.

Katika hotuba zao, viongozi hao walipiga siasa huku wakimkashifu Naibu Rais William Ruto na kuwapigia debe Bw Odinga na Bw Joho.

“Kuna mtu mmoja naweza kumwita ‘Nyale’. Nyale huyu asema anatupenda sisi Waislamu na Wapwani lakini wanapochagua mawaziri pamoja na Uhuru Kenyatta yeye hachagui Waislamu upande wake. Sisi hatutapelekwa na maneno matupu, tunataka vitendo,” alisema Bi Mboko, akionekana kumrejelea Dkt Ruto.

Bi Gedi alianza hotuba yake kwa kuomba radhi kuhusu hatua ya kuwaruhusu kuingia ukumbini, lakini akasisitiza kuwa wao ni viongozi.

“Tunaomba msahama kidogo kwa vile tumeingia ndani saa zile mmekaa nyote, lakini sisi ni viongozi wala si wanawake, samahani,” akasema.

Baadhi ya waumini wa Kiislamu walisema tukio hilo lilikuwa makosa makubwa kulingana na mafunzo ya dini ya Kiislamu ambayo kunahitajika katika jumuiko lolote lile, wanaume wawe kando na wanawake.

Waliohojiwa na Taifa Leo walisema, hafla hiyo ilihusu sherehe ya Kiislamu ya Eid ul Adha kwa hivyo kanuni za kidini zingestahili kuheshimiwa.

“Ni jambo la kuhuzunisha mno kuona kwamba, ingawa wanawake walikuwa wamekaa sehemu mbali na wanaume, wakati wa hotuba za wahusika kuanza, wanawake waliitwa na kujumuika pamoja na wanaume. Zaidi ya hayo, baadhi ya wanawake hao ni Waislamu wanaofahamu kanuni za dini,” akasema muumini aliyeomba asitajwe jina.

Wakati huo huo, Bw Joho alisisitiza atawania tikiti ya ODM ya urais dhidi ya Bw Odinga na Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya.

Baadhi ya viongozi Jumanne walikuwa wamependekeza awe mgombea mwenza wa Bw Odinga 2022.

You can share this post!

Jumwa aonywa UDA itazima nyota yake

Pigo kwa OKA Kanu ikisema haitaacha kuunga Jubilee