Habari za Kitaifa

El-Nino imeua 174 kufikia Januari, ripoti ya majanga yasema

January 5th, 2024 1 min read

NA MWANDISHI WETU

MVUA ya El Nino iliyoshuhudiwa nchini ilisababisha vifo vya watu 174; watu wazima 133 na watoto 41.

Hii ni kulingana na Kituo cha Kitaifa cha Kushughulikia Operesheni za Majanga (NDOC), kama vile El Nino.

Katika ripoti ya hivi punde, kituo hicho kinasema kuwa sekta ya kilimo pia iliathiriwa mno na mvua hiyo kubwa.

“Ekari 84,568 za ardhi ya mimea ziliharibiwa huku mifugo 6,706 ikiwemo mbuzi na kondoo wakisombwa maji. Madhara hayo yalishuhudiwa zaidi katika kaunti za Lamu, Tana River, Garissa, Mandera, Wajir, Homabay na Kitui, na kutishia upatikanaji wa vyakula maeneo hayo,” ilieleza NDOC.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo serikali imeanza juhudi za kukarabati miundombinu iliyoharibiwa na El-Nino, ikiwemo shule 7,878.

“Idadi ya watu waliopoteza makazi yao kutokana na mvua ya El-Nino ilipungua. Idara ya Mipango Maalum imesambaza zaidi ya tani 4,604.6 za vyakula kama vile mchele, maharagwe, unga na nyama ya ng’ombe kwa kaunti zilizoathirika,” ikasema.

Haya yanajiri siku chache tu baada ya Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa kutoa tahadhari kwa Wakenya watarajie jua kali na ukame kote nchini hadi mwishoni mwa mwezi huu.

Hata hivyo, nyanda za Ziwa Victoria, Bonde la Ufa Kusini, Kusini Mashariki na Pwani Kusini zinatarajiwa kupata mvua.