Habari za Kaunti

Elachi afichua Kilimani imegeuzwa danguro la vibiritingoma, wahuni

March 14th, 2024 1 min read

NA FRIDAH OKACHI

MBUNGE wa Dagoretti Kaskazini Beatrice Elachi amefedheheshwa na jinsi wasichana wadogo kutoka mitaa ya mabanda ya Kawangware na Kibra wanavyobadilisha mitaa ya kifahari katika eneobunge lake kuwa ngome kuu ya biashara ya ngono.

Mbunge huyo aliambia Taifa Leo kuwa akipita mwenye amejionea wasichana hao wakijiuza kimwili katika mtaa wa Kilimani.

“Inakuwa ni shida majira ya jioni. Saa moja jioni unapata wasichana wamefika. Kwanza wanajua ni block gani wanaenda,” akasikitika Bi Elachi.

Hali hiyo, aliitaja kuwa inaathiri wanafunzi wa shule ambao wakiona tabia za aina hiyo mbele yao, wanaporomoka kimaadili.

“Hapa Kilimani imekuwa tatizo kwa wazazi. Mtoto anakuuliza ‘mum, hawa watu wanafanya nini?’ hadi unashindwa umjibu vipi,” akasema

Licha ya wengi kushabikia uhuru wa kuvalia jinsi wakavy, yaani, my dress my choice, Bi Elachi alisema wanawake wa umri wa ujana hawafai kuvuka mipaka.

Kiongozi huyo ambaye zamani alikuwa Spika wa Bunge la Kaunti ya Nairobi, alifananisha shughuli hizo za usiku zinazofanyika Kilimani kuwa ni sawa na ‘Sodoma na Gomora’.

Mbunge wa Dagoretti Kaskazini Beatrice Elachi. PICHA | MAKTABA

Mbali na wasichana kujiuza, mbunge huyo alidai kwamba vijana wa kiume kwenye magenge ya uhalifu huhangaisha wapitanjia bila kujali.

“Usalama hapa bila walinzi na polisi ni kitu kisichowezekana. Sijui ni nini kinachoendelea katika nchi hii yetu,” alisema.

Alisema madanguro yanaongezeka kila uchao na kwamba hata raia wa kigeni kutoka Nigeria, Pakistan na China wana mitandao yao ambapo hulindwa na polisi.

Aliitaka serikali kuweka nidhamu kuhakikisha hakuna baa au madanguro karibu na makazi.

“Utapata familia na watoto wao wanakaa maisha ya kukerwa na makelele… hakuna amani. Serikali ya Kaunti ya Nairobi imekimywa. Tutaanza kuweka vikwazo kwa wapangaji na wanye nyumba ili kujali maslahi ya wakazi,” akasema.