Habari MsetoSiasa

Elachi amkataa Ann Mwenda kuwa naibu mteule wa Sonko

January 20th, 2020 2 min read

Na COLLINS OMULO

GAVANA wa Nairobi Mike Sonko amepatwa na pigo baada ya jina la Ann Mwenda aliyemteua kuwa naibu wake kukataliwa na Spika wa Bunge la Kaunti.

Bi Mwenda sasa atalazimika kungojea kwa muda mrefu kujua hatima yake.

Spika wa Bunge la Kaunti ya Nairobi Beatrice Elachi alisema kuwa Gavana Sonko alimteua Bi Mwenda bila kufuata utaratibu uliowekwa na Tume ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Wakati huo huo, Mahakama ya Juu imesema kuwa itaanza kutathmini uhalali wa uteuzi wa Bi Mwenda kuanzia Februari 6, 2020.

Kulingana na mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati, kabla ya gavana kuteua ni sharti jina lake litumwe kwa tume hiyo apigwe msasa.

Baada ya jina hilo kupokelewa, tume ya IEBC inateua afisa atakayempiga msasa mtu anayependekezwa kuwa naibu gavana.

“Baada ya kumpiga msasa tume ya IEBC itampa cheti cha uteuzi na nakala yake inatumiwa gavana husika. Baada ya kukabidhiwa cheti cha uteuzi, gavana sasa yuko huru kuwasilisha jina katika bunge la kaunti ili kuidhinishwa na madiwani,” akasema Bw Chebukati.

“Endapo mtu huyo ataidhinishwa na madiwani, spika ataandikia tume ya IEBC uamuzi wa bunge la kaunti,” anaongezea.

Tume ya IEBC baadaye itachapisha jina la Naibu Gavana katika Gazeti Rasmi la Serikali.

Tume ya IEBC pia itafahamisha Jaji Mkuu ambaye atateua jaji wa kumwapisha kwa mujibu wa Sheria ya Serikali za Kaunti.

Bw Chebukati alitoa utaratibu huo baada ya Bi Elachi kumwandikia barua akitaka kumpa ushauri kuhusu utaratibu unaofaa kufuatwa.

“Nimerejesha jina la Bi Mwenda kwa Gavana Sonko ili afuate utaratibu ufaao. Sitaki apigwe msasa na madiwani na mwishowe uteuzi huo ubatilishwe kwa kukiuka sheria,” akasema Bi Elachi.

Mahakama ya Juu ilisema kuwa uhalali wa Gavana Sonko kuteua Naibu Gavana ilhali amezuiliwa kwenda afisini hadi pale kesi ya ufisadi inayomkabili itakaposikizwa na kuamuliwa na kutathminiwa kuanzia Februari 6.

“Tunawahakikishia kuwa suala hilo likiwasilishwa katika Mahakama ya Juu, korti itashughulikia suala hilo kwa haraka na kutoa ushauri wake kwa kuzingatia sheria na Katiba,” akasema Bi Catherine Wambui, Mkurugenzi wa Uhusiano Mwema wa Idara ya Mahakama.

Bi Mwenda ni afisa mkuu wa Idara ya Kukabiliana na Mikasa Kaunti ya Nairobi na iwapo iwapo uteuzi wake utaidhinishwa atachukua nafasi iliyoachwa wazi na Polycarp Igathe aliyejiuzulu mwaka mmoja uliopita.

Bw Sonko ambaye amekuwa akihudumu bila ya naibu gavana anakabiliwa na sakata ya ufujaji wa Sh357 milioni.

Japo Bi Mwenda aliteuliwa Januari 6, mwaka huu, bunge la kaunti lilipanga kumpiga msasa mwezi ujao ili kutoa mwanya wa kupata ushauri kutoka kwa Mahakama ya Juu ikiwa uteuzi wake ni halali au la.

Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji alipinga uteuzi wa Bi Mwenda akisema kuwa Sonko alikiuka masharti aliyopewa kabla ya kuachiliwa huru kwa dhamana kwamba hatatekeleza majukumu take hadi kesi inayomkabili iamuliwe.