Habari Mseto

Elachi aongoza sherehe ya kuapishwa kwa wanachama wapya wa bodi ya huduma za bunge la Nairobi

October 25th, 2019 1 min read

Na CHARLES WASONGA

SPIKA wa Bunge la Kaunti ya Nairobi Beatrice Elachi mnamo Jumatano aliongoza hafla fupi ya kuapishwa kwa wanachama wawili wapya wa Bodi ya Huduma za Bunge la Kaunti ya Nairobi (NCASB).

Wawili hao ni diwani wa Maringo Hamza Mark Ndung’u (Jubilee) na mwenzake wa wadi ya Nairobi West Maurice Gari (ODM).

Madiwani hao walichukua nafasi ya kiongozi wa wengi katika bunge hilo Abdi Guyo (Wadi ya Matopeni) na kiongozi wa wachache Elias Otieno (Kileleshwa).

Bodi hiyo pia inashirikisha mwananchi wa kawaida aliyetueliwa na bunge hilo la kaunti kutoka miongoni mwa watu wenye ufahamu na tajriba katika uendeshwaji wa masuala ya umma.

Bi Elachi ambaye ni mwenyekiti wa bodi hiyo alimteua Bw Ndung’u kuwa naibu mwenyekiti.

Bw Guyo ambaye amekuwa akipinga kurejea kwa Elachi, hali iliyosababisha fujo katika bunge hilo wiki moja iliyopita, hakuwepo katika sherehe hiyo ya kulishwa kiapo kwa Ndung’u na Gari.

Mabadiliko

Katibu Mkuu wa Jubilee Raphael Tuju ndiye alitangaza mabadiliko kuhusu uwakilishi wa Jubilee katika bodi hiyo (NCASB).

Alisema kuwa chama hicho bado kinajadiliana kuhusu mabadiliko mengine ambayo yanafaa kufanywa katika uongozi wa bunge hilo la Nairobi kufuatia mzozo uliotokea wiki jana.

Barua kuhusu mabadiliko hayo ilitumwa kwa Bi Elachi na kunakiliwa kwa Bw Guyo, Kiranja wa wengi Chege Mwaura na Ndung’u.

Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna kwa upande wake alimteua Gari ambaye atachukua mahala pa kiongozi wa wachache Bw Otieno.

Bw Gari ni mfuasi sugu wa Elachi.

Miongoni mwa wajibu wa Bodi hiyo ni kusimamia matumizi ya fedha katika Bunge la Kaunti ya Nairobi, kukadiria mishahara na mazingira ya kazi ya watumishi wa bunge hilo na masuala mengine yanayohusiana na masilahi ya wafanyakazi wa bunge hilo na madiwani wote.