Michezo

Eldonets wachomoa wanavikapu matata kutoka vyuoni

September 25th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

KOCHA Maurice Ouma wa Eldonets amethibitisha kwamba usimamizi wa kikosi hicho kinachojisuka upya, kimejinasia huduma za wanavikapu sita kwa minajili ya kampeni za msimu ujao wa Ligi ya Shirikisho la Vikapu la Kenya (KBF).

Mbali na Humphrey Lesile na Philip Omondi walioagana na kikosi cha Chuo cha Kiufundi cha Eldoret, Eldonets wamejinasia pia maarifa ya Dennis Omache kutoka Chuo Kikuu cha Kisii na Alvin Mulupi aliyejiengua kambini mwa Chuo Kikuu cha Egerton. Wanavikapu wengine ni Anthony Mukhebi na Collins Wekesa.

Wekesa amewahi kuchezea Nairobi City Thunder Mukhebi akiingia katika sajili ya Eldonets baada ya kuhamia mjini Eldoret kutoka Nairobi.

Wekesa alikuwa sehemu ya kikosi cha Thunder kilichowakung’uta Eldonets katika mchuano wao wa kwanza wa mchujo kwenye Ligi Kuu ya Vikapu muhula uliopita.

Kwa mujibu wa Ouma, wengi wa wanasoka ambao wanasajiliwa na Eldonets kwa sasa ni wanafunzi wa vyuo vikuu mbalimbali vya humu nchini na kutoka kwa baadhi ya klabu za madaraja ya chini.

“Lengo letu ni kukamilisha kampeni za msimu ujao miongoni mwa vikosi vya kwanza,” akasema Ouma.