Makala

Eldoret inavyoendelea kuibuka kitovu cha ulaghai na utapeli

April 27th, 2024 2 min read

TITUS OMINDE NA LABAAN SHABAAN

TAHADHARI imetolewa kwa wanaonuia kununua mali na magari eneo la Eldoret kufuatia ongezeko la matukio ya ulaghai wa kibiashara.

Watapeli wa majengo mjini Eldoret wanaonekana kuelewa sana desturi ya njama za wizi na makachero wanawadadisi.

Wakora hawa hughushi stakabadhi muhimu kama vile hati za umiliki wa ardhi, vitambulisho vya kitaifa, na sahihi ya msajili wa ardhi.

Nyaraka za korti zinaonyesha, kwa kutumia kadi ya kitambulisho, wanaweza kuunda namba ya utambulisho inayotolewa na Mamlaka ya Mapato nchini (KRA).

Afisa wa polisi ambaye ni mtaalamu wa masuala ya utapeli wa ardhi anafichua watapeli wameunda vikundi vya watu maarufu.

“Hakuna tapeli wa ardhi anafanya kazi pekee yake. Wameunda mtandao wa watu wenye kazi mahususi,” alieleza akiomba kutotajwa.

Mmoja wa waathiriwa wa sakata hii ni Mhubiri John Bor ambaye alipoteza shamba na nyumba yake kwa matapeli alipokuwa amelazwa miezi mitatu kwenye chumba cha wagonjwa mahututi baada ya kujeruhiwa katika ajali.

“Nilishangaa kuona kuna mtu anamiliki shamba langu baada ya kuondoka hospitalini. Alidai kuwa aliuziwa shamba na kiongozi wa mtaa ambaye anashukiwa kughushi hati zangu zilizotumiwa katika mauzo feki,” aliambia Taifa Leo.

Bw Bor alipiga ripoti kwa Idara ya Ujasusi (DCI) kaunti ya Uasin Gishu na uchunguzi unaendelea.

Wakili wake Cheruiyot Kirui ameandikia Tume ya Maadili na Kukabili Ufisadi (EACC) akitaka kiongozi wa mtaa anayeshukiwa achukuliwe hatua za kisheria.

Bw Cheruiyot aliwasiliana na EACC kupitia meneja wa ukanda wa Bonde la Ufa Charles Rusungu.

Meneja huyu akijibu waraka huo Machi 15, 2023, aliwasilisha suala hili kwa DCI akisema linafaa kushughulikiwa na makachero sababu ni tukio la utapeli.

Takwimu za DCI zinaashiria kuwa, kila wiki Eldoret huripoti visa viwili vya utapeli.

Wanunuzi wa mashamba hulipia ardhi baada ya kuhakikisha hati katika sajili ya ardhi lakini baadaye huambiwa wamelaghaiwa.

Sakata hii pia imewaibia hata mawakili wenye tajiriba pana katika masuala ya umiliki wa mali.

Maafisa wa ardhi pia wameripotiwa kusaidia matapeli kuwaibia Wakenya.

Haya ni kulingana na mwanabiashara maarufu Eldoret, Leah Chepchumba ambaye pia amewatosa ndani maafisa wa DCI, viongozi wa serikali na mabroka wa mashamba.

Mwanabiashara huyu alifichua kuwa alimshtaki kortini mumewe (Stephen Sugut) mwaka wa 2008 kisha ‘mtu akajitokeza’ kutaka alipe Sh200,000 kama ada ya mchakato wa kesi ya ardhi.

“Nilishangaa kuona mtu ambaye si wa familia yetu akitaka kulipwa katika kesi ambayo hakuhusika,” alifunguka Bi Chepchumba.

Kauli hii ilikaririwa na afisa mmoja wa polisi ambaye hakutaka kutajwa. Alisema wahusika wakuu wa sakata hii ni maafisa wa Wizara ya Ardhi na mawakili wenye hila.

Isitoshe, alifichua kuwa walaghai aghalabu hulenga mashamba ambayo hayajastawishwa ama ya wamiliki waliofariki.

Kesi sawia imewasilishwa kortini Eldoret ambapo wanaume wawili walishtakiwa kwa kughushi vitambulisho kufanikisha uuzaji wa mashamba. Washukiwa wamepinga mashtaka.

Mnamo Jumatatu, muuzaji magari mjini Eldoret Bw Sammy Gichuhi  alifikishwa kizimbani mbele ya Jaji Mkuu Mkazi Keyne Odhiambo.

Hii ni kwa sababu ya tukio la Machi 24, 2021 aliposhukiwa kumlaghai mteja Benedetta Wairimu Nderitu kwa kughushi stakabadhi ya umiliki wa gari.

Bw Gichuhi kadhalika anakabiliwa na kesi ya kuunda hati feki kinyume cha sehemu ya 357 ya Sheria ya Makosa ya Jinai. Kesi hiyo inaendelea na itatajwa Mei 5.

Afisa Mpelelezi wa Kaunti ya Uasin Gishu (CCIO), Daniel Muleli alithibitisha kuwa visa hivi hutokea sana eneo hilo.

“Tunafanya kila tuwezacho kukabili washukiwa wote,” alisema Bw Muleli.