Makala

Elewa kilimo cha kisasa cha mapapai na mboga

September 14th, 2020 2 min read

Na DIANA MUTHEU

BAADA ya kufanya kazi ya mauzo kwa takriban miaka kumi, Enos Msungu aliamua kuacha ajira hiyo na kujitosa kwa kilimo.

Bw Msungu aliweka akiba ya Sh200,000 baada ya kununua shamba eneo la Kashani, kata ndogo ya Bamburi katika kaunti ya Mombasa, alizozitumia kuanzisha kilimo cha mboga na matunda.

Tulipofika shambani mwake mwendo wa saa sita mchana, Bw Msungu alikuwa mbioni kunyunyizia mimea yake maji.

Jinsi anavyokuza mimea yake ni tofauti na wakulima wengine katika eneo hilo. Bw Msungu amejitosa katika kilimo cha mboga zinazomea katika chupa za maji zilizokatwa katika maumbo tofauti tofauti.

Anasema alilazimika kupanda mboga katika chupa hizo baada ya kugundua kuwa mchanga katika shamba lake haukuweza kushikilia maji kwa muda mrefu.

“Jambo muhimu katika kilimo ni mchanga. Kwa miaka minne sasa nimekuwa nikichanganya mbolea ya mifugo, nyasi pamoja na mchanga katika shamba hili, angalau ipate kuwa na rotuba ya kutosha kwa mboga,” akasema Bw Msungu.

Bw Enos Msungu akionyesha baadhi ya mboga katika shamba lake. PICHA/ DIANA MUTHEU

Pia, mimea yote katika shamba hiyo inanyunyiziwa maji kwa kuwa mvua katika eneo hilo hunyesha kwa viwango vidogo.

“Miaka miwili ya kwanza baada ya kuanza kilimo, nilikuwa nateka maji katika bwawa moja lililo karibu na shamba langu. Mwaka jana, nilijikakamua na kuchimba kisima changu, namshukuru Msungu kwa kuwa haina chumvi nyingi,” akasema huku akiongeza kuwa maji ya chumvi haikuzi mimea.

Katika shamba hilo la robo tatu hekari, mboga aina ya mnavu, mkunde,mchicha, hoho, mabenda na sukuma zimepandwa.

Pia, Bw Msungu anakuza miti 200 ya mipapai, 50 ya ndizi na mihogo katika shamba lake. Aliongeza kuwa aliwahi kupanda nyanya na pia kufuga samaki.

Kwa kuwa shamba hilo liko katika eneo la milima, mkulima huyo alieleza Akili Mali kuwa alilazimika kuchimba na kusawazisha mchanga ndipo aweze kupanga chupa hizo, kisha akapanda mimea yake kutoka kwa bustani ya miche analolitayarisha mara kwa mara.

Mboga aina ya mchicha ikiwa imepandwa ndani ya chupa. PICHA/ DIANA MUTHEU

“Nilianza kupanda mboga ndani ya chupa 400 na mwaka huu, tuna chupa zaidi ya 3,000. Chupa hizi husaidia kuhifadhi maji katika mchanga msimu huu wa kiangazi,” akasema Bw Msungu.

Kaunti ya Mombasa inafahamika kuwa na viwango vya juu vya joto, hivyo mkulima huyu pia amelazimika kununua neti spesheli ili kukinga mimea yake kutokana na miale ya moja kwa moja ya jua.

“Neti hii huzuia mboga kutokana na miale ya moja kwa moja ya jua kwa asilimia 50,” akasema huku akiongeza kuwa utoaji wa magugu na kunyunyizia dawa mimea yake ni baadhi ya mambo anayoyafanya kuhakikisha zinakua haraka na zenye ubora.

Alieleza kuwa mboga hizo huchukua kipindi cha mwezi mmoja tu, kuwa tayari kuvunwa.

Mboga aina ya mnavu Zikiwa imepandwa ndani ya chupa. PICHA/ DIANA MUTHEU

Bw Msungu anasema kuwa kilimo cha mboga kimemfaidi sana huku wateja wake wengi wakiwa wanakijiji wenzake na kina mama ambao huuza mboga katika vibanda vyao.

Mkulima Hugo huuza mboga kuanzia fungu la Sh20 na zaidi, huku mapapai akiiuza kuanzia Sh50 na zaidi ukubwa wake ukizingatiwa.

“Soko ni kubwa, sisi wakulima ndio hatuwezi kulima mboga kwa wingi kwa sababu ya changamoto nyingi tunazokumbana nazo, “ akasema huku akitaja changamoto hizo kama vile mchanga wenye rotuba finyu, wakulima wengi wanakosa maji ya kunyunyizia mimea na wadudu wanaovamia mboga na matunda shambani.

Bw Enos Msungu akieleza jinsi anaendesha kilimo cha mboga zilizopandwa ndani ya chupa. PICHA/ DIANA MUTHEU

Bw Msungu alisema changamoto hizo zitapungua iwapo Wizara ya Kilimo katika kaunti hiyo itashirikiana na wakulima na kuwapa mbegu zinazoweza kustahimili hali ya hewa katika eneo hilo, watoe dawa za bure za kunyunyizia mimea, wachimbe mabwawa na pia watoe mafunzo kwa wakulima kuhusu kilimo cha sasa.

Mkulima huyu alisema kuwa ana maono ya kununua mashine za kunyunyiza mimea maji, kuongeza idadi ya wafanyikazi pale shambani na kupanda mboga zitakazoweza kutosheleza mahitaji ya watu katika eneo hilo, kila wakati.