Michezo

Elfsborg na AIK wanazochezea Wakenya zaandikisha matokeo mseto

June 26th, 2020 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

KLABU za Elfsborg na AIK wanazochezea Wakenya Joseph Okumu na Eric ‘Marcelo’ Ouma ziliandikisha matokeo mseto kwenye mechi za robo-fainali za Kombe la Uswidi (Svenska Cupen) mnamo Alhamisi usiku.

Elfsborg ilichabanga Hacken 2-1 kupitia mabao ya kiungo Rasmus Alm na beki Christopher McVey uwanjani Bravida Arena mjini Gothenburg katika mechi ambayo Okumu alionyeshwa kadi ya njano.

Kiungo Leo Bengtsson alifungia wenyeji Hacken bao la kufutia machozi. Okumu alichezeshwa dakika zote 90.

Huku Okumu akisherekea Elfsborg kujikatia tiketi ya nusu-fainali, AIK iliona cha mtema kuni mikononi mwa wenyeji Malmo ilipokung’utwa 4-1. Anders Christiansen alifunga mabao matatu yakiwemo mawili kutokana na pasi za Soren Rieks, ambaye pia alichangia goli moja, na bao lingine kutokana na pasi ya Guillermo Federico Molins Palmeiro.

Ouma bado yuko mkekani akiuguza jeraha alilopata mwisho wa mwezi Mei mazoezini.

Timu yake ya AIK ilitangulia kuona lango kupitia kwa kiungo Paulos Abraham kabla ya Malmo kujibu na mabao manne.

AIK ilikamilisha mechi hiyo watu tisa baada ya Abraham na beki Per Karlsson kulishwa kadi nyekundu.

Elfsborg itapepetana na Goteborg nayo Malmo ivaane na Mjally katika nusu-fainali hapo Julai 9. Goteborg ililipua Hammarby 3-1 katika muda wa ziada baada ya ule wa kawaida kumalizika 1-1 nayo Mjallby ilibandua Falkenbergs nje kwa kuichapa 1-0 hapo Alhamisi.