Elfsborg ya Joseph Okumu yang’aria Helsingborg msimu mpya wa Uswidi ukinukia

Elfsborg ya Joseph Okumu yang’aria Helsingborg msimu mpya wa Uswidi ukinukia

Na GEOFFREY ANENE

KLABU ya Elfsborg anayochezea Mkenya Joseph Okumu ilizoa ushindi wa pili mfululizo katika maandalizi yake ya msimu mpya wa 2021 baada ya kukung’uta wageni wao Helsingborg 1-0 uwanjani Rydahallen hapo Februari 5.

Elfsborg, ambayo ilicharaza Hacken 3-0 Januari 22 uwanjani humu katika mechi yake ya kwanza ya kujipima nguvu, ilizamisha Helsingborg kupitia bao la kiungo Rasmus Alm dakika ya 42.

Beki Okumu alichezeshwa kipindi cha kwanza pekee. Mchezaji huyo wa timu ya taifa ya Kenya aliibuka mchezaji bora wa Elfsborg aliyejitokeza kuwa muhimu msimu uliopita.

Elfsborg itakamilisha maandalizi yake na michuano ya kirafiki dhidi ya AIK anayochezea beki Eric “Marcelo” Ouma (Februari 12) na Norrkoping (Februari 16). Itaanza msimu kwa kusakata mechi za makundi za Kombe la Uswidi dhidi ya Degefors, Utsiktens na Falkenberg kati ya Februari 22 na Machi 6.

AIK pia imezamia matayarisho ya msimu mpya ambapo itakabana koo na Orebro SK hapo Jumapili katika mechi mbili za dakika 75 kila moja badala ya mechi moja ya dakika 90.

  • Tags

You can share this post!

EACC yaelezea hofu ya fedha za serikali kuporwa uchaguzi...

MIIBA TELE MBELE YA UHURU