Michezo

Elfsborg yatoka sare tasa dhidi ya Helsingborg

June 23rd, 2020 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

KLABU ya Elfsborg imeumiza nyasi bure baada ya kutoka sare tasa dhidi ya Helsingborg katika mchuano wa Ligi Kuu ya Uswidi, Jumapili.

Beki Mkenya Joseph Okumu alichezeshwa dakika zote 90 dhidi ya Helsingborg anayochezea Martin Olsson ambaye mamaye ni Mkenya.

Hapo Jumapili, AIK anayochezea beki Mkenya Eric ‘Marcelo’ Ouma ilitwanga Hammarby inayomilikiwa na gunge Zlatan Ibrahimovic 2-0 kwenye mechi ya Ligi Kuu ya Uswidi uwanjani Tele2Arena.

Ouma hakushiriki mchuano huo kwa sababu bado anauguza jeraha alilopata Mei 29 mazoezini. Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 23 alifanyiwa upasuaji Mei 30 huku klabu yake ikifichua kuwa atakuwa mkekani kwa kati ya wiki sita na wiki nane.

Kiungo Bilal Hussein, ambaye wazazi wake walihamia Uswidi kutoka Somalia, aliweka AIK bao 1-0 juu dakika ya 55. Dakika tatu baadaye, AIK iliimarisha uongozi wake hadi 2-0 kupitia kwa kiungo Sebastian Larsson aliyefuma wavuni penalti safi.

AIK itarejea uwanjani hapo Juni 28 kupepetana na miamba Malmo jijini Stockholm nayo Elfsborg itakabana koo na Orebro mnamo Juni 28.

Norrkoping iko kileleni mwa ligi hiyo ya timu 16 kwa alama tisa baada ya kushinda mechi zake tatu za kwanza.

Inafuatiwa na Kalmar na AIK, ambazo zimezoa alama sita baada ya kuzoa ushindi mara mbili na kupoteza mchuano mmoja. Malmo na Elfsborg zinafunga mduara wa tano-bora kwa alama tano kila moja.

Hammarby, ambayo Ibrahimovic alinunua asilimia 23.5 mwezi Novemba 2019, ni nambari saba kwa alama nne.