Habari

ELIMU: Kamati kupokea maoni hadi leo jioni

May 22nd, 2020 1 min read

DAVID MUCHUNGUH na OUMA WANZALA

WAKENYA wana hadi saa kumi na moja leo jioni kuwasilisha mapendekezo yao kwa kamati ya kitaifa ya elimu inayotarajiwa kusaidia Waziri kutoa mwelekeo wa wakati wa wanafunzi kurejea shuleni wakati huu wa janga la corona.

Kamati hiyo inatarajiwa hatimaye kumshauri Waziri wa Elimu, Prof George Magoha ikiwa shule zitafunguliwa Juni 4 au tarehe hiyo kuahirishwa.

Waziri anatarajiwa kuelezea Seneti juma lijalo kuhusu hatua ambazo zimepigwa kuhusiana na masomo mtandaoni huku kukiwa na hofu kuhusiana na wanafunzi kurejea madarasani janga la corona likiendelea kutatiza.

Kamati hiyo inayoongozwa na Bi Sarah Ruto imeendelea kupokea maoni kutoka kwa wadau wa elimu kuhusu wakati ambapo shule zitafunguliwa.

Seneta Maalum, Beatrice Kwamboka aliitaka Seneti kuagiza Prof Magoha kueleza hatua anazonuia kuchukua kutatua changamoto zilizopo miongoni mwa wanafunzi kuweza kusomea mitandaoni ili waweze kuwa pamoja na wenzao.

Waziri pia anatarajiwa kuelezea ikiwa wazazi watahitajika kulipa karo yote ya muhula wa pili, hasa ikibainika kuwa karo ya muhula wa kwanza haikutumika ikakamilika baada ya shule kufungwa mapema.

Bi Makori aliwasilisha pendekezo hilo kwa kamati ya elimu kufuatia taarifa kuwa baadhi ya shule za wamiliki binafsi zinawataka wazazi kulipa karo yote ya wanafunzi la sivyo watimuliwe kwa kuchelewa kulipa karo.

Alhamisi, Bi Ruto alisema atatoa taarifa baada ya muda wa kupokea maoni kumalizika leo Ijumaa.