Habari za Kaunti

Elimu: Taita Taveta yakabiliwa na uhaba wa walimu, mimba za mapema

March 28th, 2024 1 min read

NA ANTHONY KITIMO

SWALA la uhaba wa walimu na mimba za mapema kwa wanafunzi limetajwa kuwa chanzo kikubwa cha kudorora kwa viwango za elimu Kaunti ya Taita-Taveta.

Viongozi wakiongozwa na Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula, mbunge wa Wundanyi Danson Mwashako na mwenzake wa Taveta John Bwire, wameomba serikali kuu kushughilikia maswala hayo mawili ili kuboresha elimu kama ilivyokuwa siku za zamani.

Bw Mwashako alisema licha ya Kaunti hiyo kuorodheshwa kuwa miongoni mwa maeneo kame nchini, walimu wananyimwa marupurupu spesheli ya wanaofanya kazi katika mazingira magumu.

“Inasikitisha kuona ni walimu wa Mwatate na baadhi ya wale wanaofanya kazi Voi ndio wanapata marupurupu hayo. Hilo limewafanya walimu ambao hawajajumuishwa kukosa motisha ya kufanya kazi na nimewasilisha jambo hilo bungeni na ninaomba Spika lifuatiliwe,” alisema Bw Mwashako.

Spika Wetangula aliahidi kufuatilia jambo hilo naye akawapatia walimu na viongozi changamoto kuwataja wanaofanya mapenzi na watoto wa shule.

“Swala la marupurupu na uhaba wa walimu nitashughulikia lakini pia ni jukumu la viongozi kuweka wazi wanaoharibu watoto wa shule,” alisema Spika Wetang’ula.