Elimu: Trevor Osore, 15 aliyeangaziwa na magazeti ya NMG afadhiliwa na Middle East Bank

Elimu: Trevor Osore, 15 aliyeangaziwa na magazeti ya NMG afadhiliwa na Middle East Bank

NA SAMMY KIMATU

skimatu@ke.nationmedia.com

WATOTO wameshauriwa kujiepusha na makundi ya wenzao watundu ambao badala ya kujishughulisha na kusoma huwa na nia mbaya shuleni kama vile uchomaji mabweni na kushiriki migomo.

Akiongea Ijumaa, Mkuu wa kitengo cha Utawala wa Benki ya Middle East (MEB), Bw Fred Chumo amesema taasisi za benki zinashirikiana na serikali kuinua maisha ya wananchi wa kiwango cha chini kwa kuwapa mikopo.

Bw Chumo alikuwa ameongoza maafisa wanakamati wanaosimamia ufadhili wa masomo ya watoto werevu kutoka familia maskini waliokosa uwezo wa kulipa karo.

Meneja wa Middle East Bank Kenya anayeshughgulika na uzingatiaji sera, Edith Omolo (kulia), Mzee William Obadiah, Trevor Osore, Fred Chumo (Mkuu wa Kitengo cha Utawala MEB) na  Meneja wa Mikopo wa MEB, Bi Elizabeth Ong’are Elizabeth Ong’are wakiwa katika afisi za benki hiyo mnamo Februari 03, 2023. PICHA | SAMMY KIMATU

Timu hiyo ilishirikiana kufadhili elimu ya mvulana Trevor Osore, 15 yatima kutoka mtaa wa mabanda wa Mukuru-Fuata Nyayo, South B, kaunti ndogo ya Starehe.

Stori ya mwanafunzi Trevor iliangaziwa katika magazeti ya Daily Nation, Sunday Nation na Taifa Leo yanayochapishwa na kampuni ya Nation Media Group (NMG).

Meneja wa MEB, Edith Omolo amesema usimamizi wa Benki uliguswa na stori ya Trevor aliyezoa alama 306 katika KCPE 2022.

Bi Omolo aliongeza kwamba benki yao itagharimia sare na karo ya Trevor kuanzia Kidato cha Kwanza hadi Kidato cha Nne.

“Akizoa alama ya C kwenda juu katika KCSE, tutamsomesha zaidi na kumchukua kama mfanyakazi wetu hapa katika benki,” Bi Omolo akasema.

Mbali na Trevor, Bi Omolo ameambia Taifa Leo kwamba wanafadhili elimu ya zaidi ya watoto 100 tangu mpango huo uanzishwe.

Wakati wa hafla hiyo, Trevor aliandamana na babu yake, mzee William Obadiah Nyagoro, 73 ambaye huishi naye tangu kufariki kwa wazazi wake wawili.

Wazazi hao, marehemu Bi Rose Mwikali na marehemu Bw Martin Obadiah walifariki Trevor akiwa mtoto mdogo.

Uwezo wa babu yake ulilemazwa baada ya nyumba zake 44 zilizokuwa kitega uchumi katika familia kubomolewa kupisha mradi wa barabara mwaka 2021.

“Nimebakia mtu wa kuombaomba mitaani kwani nina watoto wengine wanaonitegemea ila sina uwezo wa kuwalipia karo. Nakaribisha yeyote aliye na msaada wowote kunipiga jeki nisomeshe mayatima wengine watano wanaonitegemea,” akasema.

Hafla hiyo iliyofanyika katika makao makuu ya Benki ya Middle East eneo la Milimani, Kaunti ya Nairobi ilihudhuriwa pia na Meneja wa Mikopo wa MEB, Bi Elizabeth Ong’are.

Tukichapisha habari hii, mzee Obadiah na mjukuu wake walielekea katika duka moja la kuuza sare za shule mkabala wa barabara ya River Road jijini Nairobi ili wanunue vinavyohitajika shuleni.

Trevor atajiunga na Shule ya Upili ya Kiriani iliyoko Kaunti ya Kiambu.

  • Tags

You can share this post!

Dereva Karan kuanza kutetea taji la mbio za magari kitaifa...

Petanns yafungua chuo cha kiufundi kuwasaidia vijana kupata...

T L