Habari Mseto

Elimu ya vyuoni sasa ni ya mtandaoni – Profesa Waudo

September 18th, 2020 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

CHUO Kikuu cha Mount Kenya (MKU) kimewekeza pakubwa katika vifaa vya kuwezesha masomo ya kupitia mitandaoni tangu janga la Covid-19 lilipovamia Kenya.

Naibu Chansela wa chuo hicho Profesa Stanley Waudo alisema masomo kupitia mtandao ndio mwelekeo utakaochukuliwa na chuo hiki katika siku za usoni.

“Tangu homa ya corona kuingia nchini mambo mengi yamebadilika na kwa hivyo hali ya masomo pia ni sharti ibadilike. Wanafunzi watalazimika kuzingatia masomo kupitia mitandao,” alisema Prof Waudo.

Aliyasema hayo Alhamisi akiwa chuoni humo wakati wa kuwasajili wanafunzi wapya wapatao 5,000 watakaojiunga na chuo hicho kati ya Septemba na Disemba 2020.

Alisema wanafunzi hao wapya watalazimika kupewa mwongozo mpya watakapojiunga na chuo hicho ambapo jambo la muhimu ni kuendesha masomo yao mitandaoni.

“Chuo kimewekeza zaidi katika masomo ya mtandaoni na kwa hivyo wanafunzi watakaojiunga na chuo hiki ni lazima wakumbatie mpango huo,” alisema msomi huyo.

Aliwapongeza wanafunzi hao wapya kwa kufanikiwa katika mtihani wa KCSE na kusema walifanya jambo la busara kujiunga na chuo hicho ambacho kinatoa masomo ya kutegemewa.

Alisema wakati huu wa janga la Covid-19, wanafunzi wengi walikuwa wakifuatilia vipindi vya masomo yao kupitia mtandao ambapo baadhi yao wanajiandaa kufuzu kupitia mtandao mnamo Oktoba 9, 2020.

Kulingana na mipango ya chuo hicho awamu ya 18 ya kufuzu kwa wahitimu mwaka huu wa 2020 itakuwa na idadi ya mahafala wapatao 4,000.

Wanafunzi wapya wanaotarajia kujiunga na chuo hicho wameshauriwa kufuata mkondo wa wenzao wanaojiandaa kung’atuka wiki chache zijazo.

Wanafunzi hao walihimizwa kuelewa ya kwamba watalazimika kujitegemea kupitia mitandao ili kupiga hatua zaidi katika siku za usoni.

“Tunataka wanafunzi wa chuo wawe watu wa kujitegemea kila mara wanapokuwa chuoni; na hiyo tu itatimia kupitia nidhamu,” alisema Prof Waudo.

Alisema chuo hicho kiko tayari kuwapa mwongozo wa kuwa watu wa kujituma bila kutegemea wahadhiri kila mara.

Kutokana na hayo kila mwanafunzi atakuwa na maono na hata kuwa na ubunifu wakati atakapokamilisha masomo yake chuoni.