Michezo

Eliud Kipchoge atatimka mbio za INEOS 1:59 Challenge nchini Austria na wala sio Australia

October 11th, 2019 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

BAADHI ya Wakenya wanaonekana kuchanganyikiwa kidogo kuhusu nchi itakayokuwa mwenyeji wa mbio za INEOS 1:59 Challenge ambazo nyota Eliud Kipchoge atatumia kujaribu kuwa binadamu wa kwanza kutimka mbio za kilomita 42 chini ya muda wa saa mbili Jumamosi.

Baadhi yao wamekuwa wakisema bingwa huyo mara nne wa London Marathon, ambaye pia anajivunia kutwaa taji la Berlin Marathon mara mbili na Chicago Marathon mara moja, atashiriki mbio hizo nchini Australia.

Shabiki Rahab R Gichuhi aliandika kwenye ukurasa wa Facebook wa mshikilizi huyo wa rekodi ya dunia akisema, “Nakuombea. Mungu akupe nguvu na umakinifu ili uweze kutimiza lengo lako. Kama Australia ingekuwa karibu, ningefika hapo kukushangilia.”

Ukumbi huu unakuweka wapenzi wa riadha sawa kuwa ni Austria wala si Australia itakayoandaa mbio za INEOS 1:59 Challenge hapo Jumamosi.

Austria

Nchi ya Austria inapatikana barani Ulaya. Iko kilomita 8,618 kutoka Kenya, kaskazini magharibi. Katika upande wa kaskazini, Austria inapakana na Jamhuri ya Czech na Ujerumani. Hungary na Slovakia ziko upande wake wa mashariki, Slovenia na Italia upande wa kusini na Uswizi na Liechtenstein upande magharibi.

Lugha rasmi ya Austria ni Kijerumani. Jiji kuu la Austria ni Vienna. Austria ni mojawapo ya mataifa 19 yanayotumia sarafu ya Euro.

Raia wengi nchini Austria ni Waaustria, ingawa pia kunao wale kutoka Yugoslavia iliyovunjika kuunda Bosnia & Herzegovina, Croatia, Montenegro, Macedonia, Serbia na Slovenia, Ujerumani na Uturuki.

Idadi kubwa ya raia wa Austria ni Wakatoliki. Austria ina karibu raia milioni tisa. Beki David Alaba anayesakatia miamba wa Ujerumani Bayern Munich ni mmoja wa wanamichezo nyota nchini Austria.

Australia

Nchi ya Australia iko katika bara la Oceania. Ni kisiwa kikubwa ambacho majirani wake wa karibu ni Papua New Guinea, Indonesia, East Timor, Solomon Islands, Vanuatu na New Zealand. Australia iko kilomita 14,203 kutoka Bara Ulaya. Tim Cahill, Harry Kewell, Mark Viduka na Mark Schwarzer ni baadhi ya wachezaji nyota kutokea Australia, ambayo lugha yake ya taifa ni Kiingereza. Mji mkuu wa Australia ni Sydney. Australia ina jumla ya idadi ya watu 25.5 milioni. Sarafu ya Australia ni dola za Australia.