Michezo

Eliud Kipchoge gumzo kila pembe ya dunia

October 10th, 2019 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

ZIKISALIA chini ya saa 48 kabla ya Eliud Kipchoge kutafuta kuwa binadamu wa kwanza kutimka umbali wa kilomita 42 chini ya muda wa saa mbili katika mbio za INEOS 1:59 Challenge, Wakenya wanaamini vijana kutoka Bara Afrika ndio watanufaika zaidi na ufanisi wake.

Kipchoge alitua katika eneo la mbio jijini Vienna nchini Austria mnamo Oktoba 8 baada ya kusafiri pamoja na wawekaji wake wa kasi kwenye ndege maalum ya Gulfstream G280 ambayo bei ni Sh2.5 bilioni.

Baada ya bingwa huyu mara nne wa London Marathon kuchapisha kwenye ukurasa wake wa Facebook “Inaridhisha kuona wawekaji hawa wa kasi wenye tajriba ya dunia wakijiweka tayari kunisaidia kukimbia umbali huo kwa saa moja na dakika 59”, maelfu ya mashabiki walijitokeza kumtakia mbio nzuri.

Shabiki Collins Kibet anasema mafanikio ya Kipchoge, ambaye anashikilia rekodi ya dunia ya kilomita 42 ya saa 2:01:39, yatakuwa kama mwamko mpya.

“Kinachonifurahisha zaidi ni kuwa umesalia kuwa wewe; hujabadilika licha ya kuwa shujaa. Nakutakia mema. Unawapatia mamilioni ya watoto wa Kiafrika motisha ya kujiamini. Kila la kheri bingwa. Mungu akubariki,” alichapisha kwenye ukurasa wa Facebook wa Kipchoge.

Wesley Amdany, “Kila la kheri. Weka historia kutupatia motisha. Tutafurahi sana ukifanikiwa….”

Kìprùtò Cheboi, “Nakutakia mema. Onyesha dunia kuwa mtu anaweza kutimiza ndoto yake. Ari uliyonayo inafanya kila kitu kiwezekane.”

Anyango Akora, “Kipchoge anapatia motisha kizazi ambacho kina mazoea ya kufanya uamuzi mbovu. Anatukumbusha utu na umoja wetu. Tukio kama hilo linalotufanya tukumbuke kuwa sisi ni Wakenya kwanza ni nadra.”

Kipchoge atawekewa kasi na wakimbiaji 41. Baadhi ya wawekaji kasi hao ni Wakenya Philemon Kacheran, Noah Kipkemboi, Vincent Kiprotich, Augustine Choge, Jonathan Korir, Victor Chumo na Gideon Kipketer, wazawa wa Kenya Bernard Lagat, Paul Chelimo na Shadrack Kipchirchir, ambao ni Waamerika, Brett Robinson na Jack Rayner (New Zealand), ndugu Filip Ingebrigtsen, Henrik Ingebrigtsen na Jakob Ingebrigtsen (Norway), Mande Busendich (Uganda), Tesfahun Akalnew (Ethiopia) na Julien Wanders (Uswizi).

Mbio zenyewe zimeratibiwa kufanyika Oktoba 12 kati ya saa kumi na mbili asubuhi na saa nne saa ya Kenya. Saa rasmi ya mbio itatangazwa Oktoba 11.

Katika jaribio lake la kwanza la kutimka mbio za kilomita 42 chini ya muda wa saa mbili, Kipchoge alikamilisha mbio za Nike Breaking2 kwa saa 2:00:25 mjini Monza nchini Italia mwaka 2017.

Muda huu haukutambuliwa kama rekodi ya dunia na mambo pia hayatakuwa tofauti hapo Oktoba 12.