Eliud Kipchoge na INEOS waanzisha kituo Kaptagat kukuza waendeshaji wa baiskeli

Eliud Kipchoge na INEOS waanzisha kituo Kaptagat kukuza waendeshaji wa baiskeli

Na GEOFFREY ANENE

NYOTA wa mbio za kilomita 42 Eliud Kipchoge ameingia ushirikiano na kampuni ya kemikali ya INEOS kuwa na kituo cha kukuza waendeshaji wa baiskeli katika kaunti ya Uasin Gishu.

INEOS, ambayo ina timu ya waendeshaji baiskeli wa kulipwa ya INEOS Grenadiers kutoka Uingereza (ilijukana hapo awali Team Sky na Team Ineos), itaweka akademia hiyo katika eneo la Kaptagat anakofanyia mazoezi bingwa huyo mara mbili wa Olimpiki.

Katika tovuti ya INEOS Grenadiers, mwenyekiti wa INEOS Sir Jim Ratcliffe amesema, “Kuna talanta barani Afrika ya kusisimua ya michezo iliyo na ari na tamaa na hapa INEOS tunataka kuwekeza hapo ili kuisaidia kufikia uwezo wake. Nilizuru kituo hicho cha Kaptagat nchini Kenya majuzi na nikarejea nikiwa nimeshawishika kuwa ushirikiano unaweza kufanya kitu tofauti na muhimu katika uendeshaji wa baiskeli pamoja na wanamichezo chipukizi wa Afrika.”

Mkurugenzi wa michezo wa INEOS na mkuu wa timu ya INEOS Grenadiers Sir Dave Brailsford aliongeza kuwa hatua hiyo ni maendeleo muhimu katika ulimwengu wa uendeshaji wa baiskeli. “Ina nguvu ya kuleta mabadiliko ya kudumu kwa kukuza waendeshaji baiskeli wapya kutoka Afrika… Nilijionea mwenyewe nilipokutana na wanariadha wachanga Kaptagat. Ari yao, kujitolea kwao na upendo wao kwa michezo unaendana sawa na moyo wa INEOS Grenadiers wa kujitolea kwa dhati na kutaka kuwa bora. Pamoja naamini tunaweza kupiga hatua ya kipekee na muhimu katika uendeshaji wa baiskeli nchini Kenya, Afrika na mchezo wenyewe.”

Kipchoge alisema anajivunia kuwa wanapanua kambi ya mazoezi ya Kaptagat kutoka kuwa ya riadha pekee na kuwa ya michezo. Kituo hicho kitafahamika kama INEOS Eliud Kipchoge Cycling Academy.

  • Tags

You can share this post!

Mwilu aonya wanaoendeleza ndoa za mapema Narok

Wanasiasa wajiuza kwa jina la Mungu

T L