Makala

Eliud Ndung'u Kinuthia: Rais amependekeza bunge limpitishe aongoze NPSC

February 21st, 2019 3 min read

Na MWANGI MUIRURI

BW Eliud Ndung’u Kinuthia kwa sasa yuko hatua chache tu afanikiwe ama asifanikiwe kutwaa uenyekiti wa Tume ya Huduma za Polisi (NPSC) baada ya Rais Uhuru Kenyatta kupendekeza jina lake na kuliwasilisha bungeni.

Ikiwa ataidhinishwa, atarithi hatamu za uongozi wa NPSC kutoka kwa Bw Johnston Kavuludi ambaye huduma yake ya miaka sita na ambayo kikatiba haina awamu ya pili,  ilitamatika Oktoba 2018.

Sio wengi wanamjua Bw Kinuthia ambaye ni mzawa wa Kaunti ya Lamu.

Huyu ni Mkristo ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 45.

Ikiwa atatwaa majukumu hayo katika NPSC basi atakuwa amechukua usukani katika awamu muhimu ya mabadiliko katika vikosi vya polisi.

Tayari maafisa wote wamejumuishwa chini ya huduma moja, maafisa kulipwa marupurupu ya upangaji na kutakikana waondoke katika makazi ya serikali.

Nyongeza ya mishahara

Pia maafisa wengi wamekuwa wakiitisha nyongeza ya mishahara.

Hata hivyo, Bw Kinuthia akifanikiwa atakabiliana na changamoto kama za kikosi kinachokisiwa kuenzi ufisadi, kukiwa na baadhi ya maafisa ambao hukiuka haki za kibinadamu kwa kiwango kikuu huku wengine wakizua visa vya kujitia kitanzi na pia kuwaua wakubwa wao kwa risasi wakiwa kazini.

Ufaafu wa Bw Kinuthia ulitiliwa mkazo na Katibu msaidizi katika Wizara ya Usalama wa Ndani, Amos Gathecha,  Joseph Mukui  ambaye ni katibu katika Wizara ya Mipango na Uchumi pamoja na Inspekta Mkuu wa Polisi, Joseph Boinnet ambao aliwaorodhesha kama mashahidi wa uwezo wake kikazi.

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Mpango wa Usalama wa Nyumba Kumi, Joseph Kaguthi anamtaja Bw Kinuthia kama “kijana ambaye ari yake na kujituma kuhudumia taifa lake sio ya kuiga bali ni kama mwito.”

Ana Shahada ya Elimu zingatio likiwa ni Takwimu kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi (1999) na ile ya uzamili kuhusu Masuala ya Kimaendeleo na Jinsia kutoka chuo chicho hicho (2006).

Pia ana Shahada ya Uzamili kuhusu biashara kutoka Chuo Kikuu cha Strathmore (2015).

Kabla ya kuteuliwa kwake, Bw Kinuthia alikuwa akihudumu kama mshauri wa NPSC kuhusu sera za mageuzi na ambapo ni mwandani wa ratiba ya mageuzi yanayokusudiwa kutekelezxwa ndani ya kikosi cha polisi kabla ya 2020.

Kwa walio na ufahamu wa matukio ya kisiasa, watakumbuka kuwa huyu Kinuthia alitangaza kuwania ugavana wa Kaunti ya Lamu 2017 lakini kabla ya kuyavulia nguo ayaoge kwa uhakika, akasuasua.

Mambo yalianza kujipa taswira ya merikebu iliyokuwa ndani ya mawimbi makali baada ya aliyekuwa mgombea wake mwenza kukosa kuafikia vigezo vya kisheria kuhusu stakabadhi za elimu na akakosa kuidhinishwa.

Hilo lilikuwa na maana kuwa uwaniaji wa Bw Kinuthia haungeidhinishwa bila mgombea mwenza aliyehitimu na ndipo alimtema huyo James Matole Tuva na akamteua Bw James Mwangi.

Hata hivyo, siku 48 kabla ya kujitosa kwa debe la Agosti 8, 2017, Bw Kinuthia aliandaa kikao na wanahabari na akatangaza kuwa Rais Uhuru Kenyatta alikuwa amempigia simu na ambapo baada ya kujadiliana kwa dakika 20, akaona “haidhuru bora nitupilie mbali azma ya kugombea ugavana katika Kaunti ya Lamu.

“Rais amenihimiza kuwa ikiwa chama cha Jubilee kitashinda uchaguzi mkuu ujao, name nijiondoe na niunge mkono mwaniaji wa ugavana hapa Lamu kwa tiketi ya Jubilee Bw Fahim Twaha, basi mimi na uwaniaji wangu wa PNU tutatuzwa na kazi nyingine mbadala ya uongozi,” akasema.

Alisema kuwa hakuwa na shaka yoyote kuwa Rais alikuwa na nia njema kwake na ndipo alikubali kujiondoa.

Kujiondoa kwake kulimwacha aliyekuwa akisaka awamu ya pili kama gavana wa Lamu, Bw Issa Timamy wa Amani National Congress (ANC), Abdalla Fadhil wa Orange Democrtatic Party (ODM) na Swaleh Imu wa Wiper party wakimenyana na ambapo hatimaye ujumlishaji ulimweka Twaha kidedea.

Kwa sasa, Bw Kinuthia anashikilia kuwa hata ingawa Rais alimwahidi kazi ikiwa Twaha angetwaa wadhifa huo wa Lamu, kazi hii ya NPSC sio ya kutuzwa kisiasa.

“Nilikuwa naingoja hiyo ya kuahidiwa lakini nikatuma ombi kuhusu hii ya NPSC. Nilimenyana na majina tajika, mmojawapo wao akiwa ni aliyekuwa Spika wa Bunge la Kitaifa, Kenneth Marende. Hatimaye nimeishia kufaulu. Hii kazi sio ya kutuzwa, bali ni ya kung’ang’ania,” asema akiwa na matumaini makubwa ya kuidhinishwa.