Habari Mseto

ELIZABETH MARONGA: Utalia mwenyewe ukikubali kuigiza bila mkataba

February 19th, 2019 2 min read

Na JOHN KIMWERE

ALIANZA kushiriki uigizaji tangu akiwa mwanafunzi wa Darasa la Pili na kuamini kwamba ingekuwa rahisi kwake kupata ajira katika sekta ya filamu baada ya kukamilisha masomo.

Hata hivyo ndoto yake hiyo imebakia stori tu licha ya kutangamana na waigizaji wengi tu wa nguvu.

Elizabeth Nyanchera Maronga ni miongoni mwa waigizaji wa kike wanaoibukia waliowahi kushiriki filamu kadhaa na maprodusa wao kuingia mitini bila kuwapa haki yao.

”Sitawahi kusahau kazi niliyofanya chini ya kundi la Tamasha Arts na kupigwa chenga na waajiri wetu licha ya filamu kupeperushwa kupitia kituo cha Mbugi TV,” anasema na kuongeza kuwa wenzake waliomshtumu kwa kupiga kelele akilalamikia kutofurahi baada ya kuanza kurekodi muvi bila kuandikiana mkataba na mwishowe walibakia kusaga meno.

Chipukizi huyu anasema hawakulipwa chochote kufikia siku ya leo ingawa filamu hiyo ingali inayonyeshwa.

”Ili kuepuka kutumbukia katika shimo la viongozi walafi wamiliki wa makundi tofauti ya kutengeneza muvi, kabla msanii hajaanza kazi anastahili kuandikiana mkataba na wahusika,” anasema na kudai tukio hilo lilimtia nguvu zaidi ambapo hawezi rekodi filamu yoyote kabla ya kuandikiana mkataba na wahusika.

Anasema ni jambo linaloponda msanii kutolipwa licha ya kufanya kazi nzuri pia kugharamikia mahitaji mbali mbali ili kufanikisha shughuli za kurekodi filamu.

”Nakumbuka tulirekodi filamu ya ‘Hisia’ ndani ya siku saba na lokesheni tulitumia nyumba yangu lakini Tamasha Arts hawaligharamia chochote wasanii hatutulipwa chochote,” anasema.

Anashauri wasanii chipukizi kwamba kuandikiana mkataba ni jambo nzuri maana ni rahisi kuelekea mahakamani wakati wahusika wamekataa kutoa posho.

Dada huyu ambaye kisanii alifahamika kama ‘Bella’ kwenye filamu ya ‘Hisia’ anachana maprodusa ambao hupenda kushusha wasanii wa kike hasa kutaka kimapenzi ili kuwasaidia kupata ajira.

Kadhalika anasema amegundua ni ugonjwa unaotesa bindamu wengi, huku akinukuu madai yaliyoibuliwa na mwigizaji mzawa wa hapa Kenya, Lupita Nyong’o anayetamba katika tasnia ya filamu za Hollywood.

Baada ya pandashuka hizo, baadaye Nyanchera 27 alibahatika kupata nafasi kufanya kazi na kikundi kiitwacho, ‘Nuru Lutheran Media’ ambapo alishiriki tangazo ambalo hupeperushwa kituo cha redio stesheni cha Egesa FM.

”Tulifanya Episodes 14 ambapo tunatarajia kutengeneza zingine kuendeleza shoo hiyo,” aliliuambia ukumbi huu na kusema alipendezwa sana kufanya kazi na kundi hilo maana walipewa chao baada ya kumaliza kurekodi.

Binti huyu ameolewa na kujaliwa watoto wawili anaposema kuwa msichana wake mwenye umri wa miaka mitatu ameibuka kichaa katika uigizaji.

”Ni mtoto mdogo ila hufanya vituko vya wakomavu maana nimekuwa nikienda kurekodi filamu naye,” akasema na kudai mtoto huyo anaufahamu tosha kufanya tangazo lolote kwa lugha ya Gusii pia kiswahili.

Ingawa hajashika mashiko dada huyu anasema angependa sana kuikuza talanta yake kufikia upeo wa mwigizaji wa nyumbani Lupita Nyong’o anayefanya kweli katika filamu za Hollywood.

Kimataifa anasema huvutiwa na kazi zake mwigizaji wa Nigeria, Patience Ozokwor maarufu kama Mama G.

Anavitaka vyombo vya habari kuzipatia muvi za nyumbani kipau mbele ili kuinua wasanii wanaokuja kama yeye na wengineo.

Pia anawaambia wenzake wakishiriki uigizaji wanastahili kufanya kazi kwa kujitolea mhang’a ili kutambulisha uwezo wao. Na kama haitoshi anashauri chipukizi wenzake wawe wabunifu katika sekta hiyo.