Habari Mseto

Elungata awaonya walanguzi wa dawa za kulevya

November 13th, 2019 2 min read

Na KALUME KAZUNGU

MSHIRIKISHI wa Usalama Ukanda wa Pwani, John Elungata, ametoa onyo kali kwa walanguzi wa dawa za kulevya wanaonyemelea maafisa wa usalama na kuwadhuru katika harakati zao za kuendeleza biashara haramu ya mihadarati, akitaja kuwa siku zao zimehesabiwa.

Hii ni baada ya kubainika kuwa afisa wa polisi wa cheo cha konstebo, Hesbon Okemwa Anunda, ambaye mwili wake ulipatikana umetupwa kichakani eneo la Kizingitini mnamo Oktoba 5, 2019, aliuawa na walanguzi wa dawa za kulevya.

Bw Elungata amefichua kuwa walanguzi hao wa mihadarati ndio waliompigia simu afisa huyo na kumdanganya kwamba kulikuwa na mshukiwa wa mihadarati aliyehitaji kukamatwa na afisa huyo.

Alisema punde afisa alipofika eneo husika, maadui walimgeukia na kumuua na kisha kutoroka na bunduki yake.

Bw Elungata alisema wanafuata kwa karibu ripoti za ujasusi kuhusiana na mauaji hayo na kwamba hivi karibuni watyawatia mbaroni wote waliohusika na mauaji hayo.

Alilaani vikali mauaji ya afisa huyo na kuitaka jamii kushirikiana vilivyo na maafisa wa usalama ili kuona kwamba wahalifu waliotekeleza unyama huo watambuliwa ili sheria ifuate mkondo wake.

Bw Elungata aidha ametaja kuwepo kwa kundi fulani linaloendeleza biashara haramu ya mihadarati eneo la Lamu Mashariki na akatangaza vita vikali dhidi ya wote wanaohusika na usambazaji na utumiaji wa dawa za kulevya Lamu na Pwani kwa jumla.

“Ninawashukuru wananchi wa hapa Lamu. Mmekuwa mkishirikiana vyema na walinda usalama ili kudhibiti usalama na amani eneo hili. Kuna kile kisa cha kuuawa kwa afisa wa polisi eneo la Kizingitini. Tunafahamu kwamba waliomuua afisa huyo ni walanguzi wa dawa za kulevya. Walimdanganya kwamba kuna mhalifu aliyehitaji kukamatwa na kisha kumvizia na kumuua. Hao ndio waliochukua bunduki yake ambayo hadi sasa haijapatikana. Ningeomba wananchi wa hapa kushirikiana nasi ili kumaliza mihadarati eneo hili na Pwani kwa jumla. Pia kuna haja ya nyinyi wakazi kusaidia polisi ili bunduki iliyopotea ipatikane,” akasema Bw Elungata.

Ametaja Lamu na Tana River kuwa kaunti ambazo bado ziko nyuma kimaendeleo na hata katika suala zima la usalama ikilinganishwa na kaunti zote sita za Pwani.

Amesema azma yake ni kuhakikisha changamoto zote zinazokabili kaunti hizo mbili, ikiwemo suala la usalama zinatatuliwa vilivyo ili iwe rahisi kwa maendeleo kuafikiwa pia kwenye maeneo hayo.

“Kaunti za kule upande mwingine wa Pwani ziko shwari kabisa. Kwa sasa changamoto zinazofaa kukabiliwa ziko Lamu na Tana River. Tunang’ang’ana ili kuona kwamba matatizo hayo yametatuliwa. Ikiwa Lamu na Tana River zitafikia maendelea, hiyo itamaanisha Kenya nzima itakuwa imeendelea vilivyo,” akasema Bw Elungata