Habari MsetoSiasa

Embakasi na Ugenya tayari kuchagua Wabunge wapya

April 4th, 2019 2 min read

NA CECIL ODONGO

WAPIGAKURA katika maeneobunge ya Embakasi Kusini na Ugenya Ijumaa wanatarajiwa kumiminika katika vituo mbalimbali vya kupigia kura kuwachagua wabunge wao baada ya kukamilika kwa muda wa kampeni mnamo Jumanne.

Katika eneobunge la Embakasi Kusini, watu 150, 314 waliojiandikisha kama wapiga kura wanatarajiwa kufika kwenye vituo 221 vya upigaji kura kuanzia saa 12 asubuhi hadi saa 11 jioni.

Kulingana na Afisa Mkuu Msimamizi wa uchaguzi huo Abdikadir Abdulahi, Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka(IEBC) jana ilisambaza vifaa 300 vya kielektroniki, masanduku na karatasi za kupiga kura katika vituo vyote vya uchaguzi.

Bw Abdulahi vile vile alitangaza kuwa maafisa 400 wa polisi wametumwa kwenye vituo mbalimbali huku wengine 40 wakikita kambi katika kituo kikuu cha kujumuisha matokeo katika Taasisi ya Mafunzo ya Chaminade mtaani Mukuru kwa Njenga.

“Maandalizi yote yamekamilika na tunaendelea kusambaza vifaa vyote hitajika kwa vituo vyote hapa Embakasi Kusini. Maafisa wetu wa usalama wapo imara kusimamia uchaguzi na tunawaomba waajiri wawape ruhusa wapigakura kutekeleza haki yao ya kidemokrasia,” akasema Bw Adulahi.

Kiti hicho kimewavutia wagombeaji 15 ingawa kivumbi kikali kinatarajiwa kati ya mgombeaji wa chama cha ODM Irshad Sumra na aliyekuwa mbunge Musili Mawathe anayewania kwa tiketi ya chama cha Wiper. Mahakama ya Juu ilifutilia mbali uchaguzi wa Bw Mawathe ambaye alitwaa kiti hicho kutoka kwa Bw Sumra katika uchaguzi wa 2007.

Wapigakura katika eneobunge la Ugenya vile vile watachagua mwakilishi wao kwenye Bunge la Kitaifa leo. Kiti hicho kimevutia Christopher Karani wa ODM, David Ochieng wa MDG, Brian Omondi wa Thirdway Alliance na Daniel Juma wa GDP.

Bw Karani na Bw Ochieng’ watatoana kijasho kwa mara nyingine baada ya Bw Karan kumshinda mpinzani wake wakati wa kura ya 2017 lakini ushindi huo ukabatilishwa na Mahakama ya Juu mwaka jana.

Msimamizi Mkuu wa Uchaguzi huo Vincent Saitabau jana alisema matayarisho yote yamekamilika huku akifichua kwamba IEBC itawafikisha kortini watu 6, wawili kwa kuendesha kampeni baada ya makataa yaliyowekwa na wengine kwa kuzua ghasia wakati wa kampeni.

Uchaguzi huo mdogo pia unatarajiwa kufanyika katika Wadi ya Lelan, Kaunti ya Marakwet na umewavutia wagombeaji watano. Ulitokana na kifo cha aliyekuwa mwakilishi wadi Vincent Tanui mwaka jana.

Wawaniaji hao ni Salome Biwott wa Kadu Asili, Timothy Kemboi wa Maendeleo Chap Chap, Pius Rotich wa CCM, Priscila Kurgat wa Jubilee na Philip Kiptanui wa GDDP.