Habari za Kitaifa

Embakasi: Serikali yawataka raia kuchukua tahadhari kuu

February 2nd, 2024 2 min read

NA CHARLES WASONGA

SERIKALI imetangaza kwamba inaendelea kufanya kila iwezalo kuwasaidia waathiriwa wa moto kutokana na mlipuko wa gesi katika mtaa wa Mradi, eneo la Embakasi, Kaunti ya Nairobi mnamo Alhamisi usiku.

Mkasa huo ulitokea saa tano na nusu usiku.

Naibu Rais Rigathi Gachagua alisema hayo Ijumaa, huku aikiyaomba mashirika ya kibinafsi na wasamaria wema pia kujitokeza kusaidia.

“Tunafanya tathmini kutambua wanaohitaji msaada wa dharura kufuatia mkasa huu,” akasema Bw Gachagua.

Awali msemaji wa serikali Isaac Mwaura alifika katika eneo la mkasa ambapo alithibitisha kuwa watu watatu wamepoteza maisha na wengine 280 wakajeruhiwa vibaya katika mkasa huo wa mlipuko wa mitungi ya gesi.

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari Ijumaa asubuhi Dkt Mwaura alisema kuwa watu hao watatu walikata roho walipokuwa wakihudumiwa katika hospitali karibu na eneo la tukio.

Aidha, msemaji huyo alikana madai kuwa mlipuko huo ulitokea katika kituo kimoja cha kujaza gesi kilichoko mtaani humo, akisema mitungi iliyolipuka ni ile iliyokuwa imebebwa na lori moja.

“Mlipuko uliotokea Alhamisi saa tano na dakika 30 za usiku katika eneo la Mradi, Embakasi, Nairobi ulitokea katika lori moja lilikuwa limepakiwa mitungi ya gesi. Moto mkubwa ulitokea na kuenea haraka,” Dkt Mwaura akaeleza.

Msemaji huyo wa serikali aliongeza kuwa mitungi ya gesi ilipaa angani na kugonga bohari la Oriental Godown lililo karibu na likateketea. Shughuli ya ushonaji na uuzaji nguo huendeshwa ndani ya bohari hilo.

Mali ya thamani kubwa–yakiwemo magari na maduka–iliharibiwa katika mkasa huo.

“Moto huo pia ulienea hadi katika nyumba za makazi na inasikitisha kuwa idadi kubwa ya wakazi walikuwa humo kwa sababu ilikuwa saa za usiku,” akaongeza.

Miongoni mwa waliojeruhiwa, 21 wanatibiwa katika Hospitali Kuu ya Kenyatta (KNH), 160 katika Hospitali ya Mama Lucy, 19 katika Hospitali ya Mbagathi, 14 katika Hospitali ya Modern Komarock huku wanane wakitibiwa katika Hospitali ya Nairobi West.

Dkt Mwaura alisema eneo la mkasa limewekwa ua na kituo cha ushauri kuanzishwa ili kushirikisha shughuli za uokoaji miongoni mwa nyingine.

“Kwa hivyo, raia wanaonywa kutokaribia eneo hilo ili kutoa nafasi kwa wahudumu wa asasi za uokoaji kuendelea na shughuli zao pasina kutatizwa,” akasema.

Msemaji huyo pia amezishukuru asasi za serikali na zile za kibinafsi ambazo zilichukua hatua ya haraka kutoa usaidizi kufuatia mkasa huo.

“Serikali inashukuru asasi hizo kama vile Huduma ya Polisi Nchini (NPS), Serikali ya Kaunti ya Nairobi, Shirika la Msalaba Mwekendu, Shirika la Kutoa Huduma za Ambulansi la St John na wasamaria wema wengine kwa kutoa huduma za dharura. Huo ndio moyo wa utaifa na uzalendo,” akasema.