Bambika

Embarambamba akubali kurudi kwa laini

March 9th, 2024 2 min read

NA FRIDAH OKACHI

MWANAMUZIKI wa Injili Christopher Nyangwara Mosioma almaarufu ‘Embarambamba’ amesema anaacha kuvalia mavazi ya kike katika video zake.

Alichukua hatua hiyo baada ya kukutana na viongozi kutoka eneo la Kisii walioahidi kumpa sapoti kukabiliana na maagizo mazito kutoka kwa Bodi ya Uainishaji wa Filamu Nchini (KFCB).

Kwenye mahojiano ya kipekee na Taifa Leo mnamo Ijumaa, Embarambamba alisema uamuzi huo wake wa kuanza kuvalia nadhifu unatokana na ‘noma’ ya masharti ya kufuta video na picha zote zisizo za staha kwenye kurasa zake na akaunti za mitandao ya kijamii.

“Niliambiwa kuvalia jinsi ile kunaashiria uovu na pia kunaenda kinyume na muziki wa Injili pamoja na utamaduni wetu wa Kiafrika. Unajua mimi ni msanii wa jina kubwa hivyo nilichanuliwa kuvalia vile kunaleta aibu kwa familia,” akasema Embarambamba.

Pia alifichua kumbe wanawe hawakuwa wakifurahia maudhui aliyokuwa akichapisha.

“Wakati mwingine watoto wangu walikuwa wakiona kwenye simu yangu video na picha za aina ile na hawakuwa wanafurahia. Lakini ilikuwa njia ya kutafuta mapato,” akaongeza.

Kwenye chaneli ya YouTube (Embarambamba Msanii) alilazimika kufuta nyimbo 500 ambazo alifanya video akiwa na mavazi ya kike.

Pia, nyimbo hizo zilihusika na matamshi machafu ambayo aghalabu yalikera wafuasi na wafuatiliaji wake.

Nyimbo ambazo zilimulikwa ni ‘Yesu Nimwagie’, na ‘Niko Uchi’ ambapo aliambiwa ili kuzirejesha mtandaoni, ni lazima atoe matamshi machafu miongoni mwa usafishaji mwingine.

“Jana (Alhamisi) nililazimika kuondoa nyimbo ambazo nilirekodi nikiwa nimevalia mavazi ya kike. Inasikitisha kuwa nitapoteza pesa kutokana na muda wa kutazamwa video hizo (views) kupungua,” alisema.

Alisema alipoteza mashabiki wa kitaifa na kimataifa.

“Nilipoteza mashabiki  kutoka kwa nchi 20 waliokuwa wakitazama mambo ambayo niikuwa ninafanya. Ni nchi 90 ambazo zilikuwa zikifanikisha mapato yangu. Utapata pale nilikuwa nikipata Sh10,000 kila mwezi sasa jinsi mambo yalivyo huenda nitatoka sufuri,” akalia.

Mwanamuziki huyo mwenye utata alisema baada ya kupokea barua kutoka KFCB ikimuamuru kulipa kiasi cha Sh6 milioni, aliona ni vyema akae na wakuu wake kujitetea.

Lakini kabla ya kufika huko, alipokea simu kutoka kwa wakili Dastan Omari na viongozi wengine wakimtaka kumpeleka.

“Nilipata afueni viongozi wa nyumbani kunipigia simu na kutaka niandamane nao kumuona Afisa Mkuu Mtendaji Dkt Ezekiel Mutua,” aliongeza.

“Nilikuwa na mawazo tele ni wapi ningetoa pesa. Mimi mwenyewe ni mtoto wa kuzaliwa na kulelewa kwa kina mama. Tunaishi naye katika nyumba moja iliyo na vyumba viwili. Mama mzazi anatumia chumba kimoja huku mimi na mke wangu tukitumia kingine. Watoto wanatumia chumba cha kupikia.  Hatuna shamba na sikujua ningetatoa wapi pesa,” akaweka mambo wazi.

Mnamo Alhamisi, Bw Omari na mbunge wa Mugirango Kusini Silvanus Osoro walijitokeza kumsaidia kusuluhisha mzozo wake na KFCB.

Bw Osoro pamoja na Bw Omari walimkutanisha Embarambamba na wawakilishi kutoka KFCB pamoja na Shirika la Hatimiliki za Muziki Nchini (MCSK) ili kutafuta suluhu muafaka kuhusu kile alichoagizwa kufanya.