Bambika

Embarambamba aomba ‘Style Mpya’

January 16th, 2024 1 min read

NA WANDERI KAMAU

MWANAMUZIKI Chris Embarambamba, ameendelea kuzua utata, mara hii, akitoa wimbo ‘Style Mpya’ ambapo anaomba staili au mbinu mpya ya kuhubiri Injili. 

Embarambamba alitoa wimbo huo Jumatatu, Janauari 15, 2024, na kuupakia kwenye mtandao wa YouTube.

Kufikia saa tisa na robo mnamo Jumanne, wimbo huo ulikuwa umetazamwa zaidi ya mara 9,110 kwenye mtandao huo, ijapokuwa umezua migawanyiko ya kihisia kuhusu ikiwa ni wa injili ya kweli au mbinu ya kutafuta ushabiki.

Tangu mwaka 2023, mwanamuziki huyo amekuwa akizua utata, kwa kutoa nyimbo kama ‘Panua’, ‘Nataka Kunyonywa’, ‘Nimwagie’ kati ya nyingine nyingi.

Anasema kwenye wimbo huo mpya: “Naomba staili mpya ili niweze kueneza injili.”

Hata hivyo, baadhi ya watu walisema kuwa baadhi ya semi anazotumia kwenye nyimbo zake ni za kisherati, na haziashirii maana halisi ya injili.

“Maana fiche ya baadhi ya semi anazotumia ni ya kisherati,” akasema Bi Risper Monsioma.

Hata hivyo, mwanamuziki huyo amekuwa akishikilia kuwa lengo lake ni “kuleta msisimko mpya katika nyimbo za injili”.

Kabla ya hapo, alikuwa pia ametoa kibao ‘Nimwagie’, ambacho pia alidai ni cha injili, na lengo lake kuu ni kumtukuza Mungu.

Licha ya ukosoaji ambao amekuwa akipokea kutoka kwa mashabiki wake kutokana na majina anayoyapa nyimbo zake, mwanamuziki huyo alisema atafanya kila awezalo kuhakikisha amezua gumzo miongoni mwa mashabiki.

Kando na semi hizo, pia huwa anatumia mitindo tata ya uimbaji, kama vile kupanda miti, nyumba au hata kuwafukuza watu na wanyama.

“Niko tayari kufanya lolote ili kuwateka mashabiki wangu. Hivyo, huwa sijali yanayosemwa kunihusu,” akasema mwanamuziki huyo.