Habari

'Embrace' wazuru JKUAT kujifunza mawili matatu kuhusu kilimo na ufugaji

July 10th, 2019 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

VUGUVUGU la akina mama katika ulingo wa siasa la ‘Embrace’ lilizuru Chuo Kikuu cha Mafunzo ya Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta  (JKUAT), Juja kwa lengo la kuangazia umuhimu wa kuhifadhi chakula.

Huku wakiongozwa na Mwakilishi wa Wanawake wa Kiambu Bi Gathoni Wa Muchomba, kikundi hicho kimetangaza wazi kuwa kinashabikia vilivyo ajenda nne kuu za serikali na handisheki ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga.

Walisema Jumanne kuwa lengo lao kuu ni kujionea jinsi JKUAT inavyoendesha maswala yake ya utafiti kuhusu chakula ili nao waweze kupeleka ujumbe huo mashinani.

“Tumefika hapa ili kupata ujuzi zaidi jinsi uhifadhi wa chakula unavyoendeshwa, halafu baadaye nasi tuteremshe ujumbe huo mashinani,” alisema Bi Wa Muchomba.

Alisema wakiwa JKUAT walijionea mambo mengi yanayostahili kusambazwa vijijini ili mwananchi wa kawaida aweze kujitegemea kwa chakula.

Alisema kuna ufugaji wa samaki, kuku, kilimo cha kuzalisha matunda, mboga na vingine vingi ambapo juhudi zikifanywa za kufuatilia mbinu za bora, bila shaka Kenya itapiga hatua katika kilimo na ufugaji.

Naye Gavana wa Kirinyaga Bi Anne Waiguru, ambaye alishangiliwa kwa vifijo alipowasili ukumbini JKUAT, alisema umefika wakati wanawake wapewe nafasi katika uongozi.

Alipendekeza kuwa na kura ya maamuzi ili ifikapo wakati wa ugavi wa mamlaka mambo yawe sare ya 50 kwa 50 bila kubagua.

“Iwapo Rais atakuwa mwanamume bila shaka ni vyema mwanamke kuwa naibu wake. Hata kama ni kiti cha waziri mkuu mpangilio uwe uo huo,” alisema Bi Waiguru.

Mkutano huo ulijumuisha wanawake wapatao 34 kutoka kaunti zote za Kenya na ambao walionekana wamevalia nguo zao nyeupe na zambarau.

Baadhi ya viongozi waliohudhuria hafla hiyo ni Rachael Shebesh, Pamela Odhiambo (Migori), Naisula Leisuuda (Samburu), Rose Buyu (Kisumu), Gladys Wanga (Homa Bay), Eve Obara (Kasipul Kabondo), Sabina Chege (Murang’a) na Beatrice Elachi (Spika) Nairobi.

‘Embrace Kenya’. Picha/ Lawrence Ongaro

Bi Sabina Chege aliwasahauri wananchi wazingatie sana ukuzaji wa chakula aina ya kienyeji kama viazi, mihogo, na ufugaji wa samaki ili kuhifadhi chakula wakati wa kiangazi.

Alisema maradhi na hasa saratani ‘inatumaliza’ kwa sababu ya vyakula vinavyowekwa kemikali na kwa hivyo ni vyema kurejelea vyakula vya kienyeji.

Alisema wao kama vuguvugu la kikundi cha ‘Embrace’ watazuru kila eneo nchini ili kuwahamasisha wanawake umuhimu wa kurejea shambani.

“Imefika wakati tujitegemee wenyewe katika ukuzaji wa chakula na tuachane na mtindo wa kuagiza chakula aina ya mchele, machungwa na mayai kutoka nchi za nje. Tuanze kujitegemea kabisa kwa lengo la kuafikia ajenda nne mojawapo ikiwa uhifadhi wa chakula,” alisema Bi Chege.