Makala

EMBU: Kiwanda kipya cha kahawa kuimarisha maisha ya wakulima

January 21st, 2019 2 min read

Na GEORGE MUNENE

WAKULIMA wa kahawa katika Kaunti ya Embu huenda wakapata afueni baada ya kiwanda kitakachonunua kahawa moja kwa moja kutoka kwao,kujengwa.

Kiwanda hicho kitaondoa madalali ambao wamekuwa wakinunua kahawa kutoka kwa wakulima kwa bei duni.

Kiwanda hicho kinachojengwa kupitia ufadhili wa serikali ya kaunti na vyama vya ushirika vya wakulima, kinatarajiwa kukamilika mwezi ujao.

“Kiwanda hicho kitakapoanza kazi wakulima watauza mazao yao moja kwa moja na kulipwa papo hapo. Huu utakuwa mwisho kwa wakulima kuuza mazao yao kwa bei duni,” akasema Gavana Martin Wambora.

Alisema kuwa wakulima watauza mazao yao kwa Sh100 kwa kilo ya kahawa.

Gavana Wambora alisema kuwa kaunti ya Embu ndiyo huzalisha kahawa ya ubora wa juu zaidi nchini ilhali wakulima wanaendelea kuhangaika kwa kuuza mazao yao kwa bei duni.

“Kahawa itanunuliwa moja kwa moja kutoka kwa wakulima kuandaliwa na kisha kuuzwa katika soko la kimataifa kuhakikisha wakulima wanajipatia faida,”akasema Bw Wambora.

Alisema kuwa kahawa hiyo haitauzwa humu nchini kwa njia ya mnada.

“Kahawa yetu ina ubora wa juu lakini sasa inatumiwa kuchanganya na kahawa duni kutoka maeneo mengine. Hilo halitafanyika tena chini ya uongozi wangu,” akasema.

Bw Wambora alisema serikali ya kaunti imechangia jumla ya Sh28 milioni katika ujenzi wa kiwanda hicho.

“Huu ni mradi muhimu na hiyo ndiyo maana serikali ya kaunti ilishirikiana na vyama vya ushirika kujenga kiwanda katika eneo la Kavutiri,” akasema.

Wakulima wa kahawa wameelezea furaha kuhusiana na kiwanda hicho ambacho huenda kikainua mapato yao.

“Tunaunga mkono mradi huo kwani utatuokoa kutoka mikononi mwa wafanyabiashara walaghai ambao wamekuwa wakinunua kahawa yetu kwa bei duni,” akasema Bw Njeru Njoka.

Wakulima hao walilalama kuwa wamekuwa wakipunjwa na wafanyabiashara hao walaghai ambao wamekuwa wakinunua mazao yao kwa bei duni.

“Tumekuwa tukiuza kahawa yetu kwa bei duni na kutusababishia hasara. Maisha yamekuwa magumu kwetu kutokana na ukosefu wa soko wa kahawa yetu,” akasema Bi Mary Wanja.