Michezo

Emery imani tele Arsenal itatinga Nne-bora

April 16th, 2019 1 min read

NA CECIL ODONGO

MKUFUNZI wa Arsenal Unai Emery anaamini kwamba timu hiyo ina uwezo wa kumaliza katika mduara wa nne bora baada ya kuichapa Watford 1-0 ugenini mnamo Jumatatu April14.

Arsenali walipanda hadi nafasi ya nne kwenye msimamo wa jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza(EPL) kwa alama 66, alama moja nyuma ya nambari tatu Tottenham Hot Spurs.

“Nafasi yetu kwenye jedwali la EPL ni muhimu sana. Sasa mambo yapo mikononi mwetu na tunaweza kubomoa au kuimarisha uwezo wetu wa kutinga nne bora mwishoni mwa msimu,” akasema Emery ambaye alikuwa kocha wa zamani wa PSG ya Ufaransa na Sevilla ya Uhispania.

“Tulikuwa tukicheza na kumlazimisha kipa wao kurejea langoni mwake kila mara. Bao la Aubameyang lilikuwa zuri sana ikizingatiwa lilitokana na masihara ya mnyakaji wa Watford,” akaongeza Emery.

“Nafikiri tulidhibiti mechi vilivyo na kwa kuwa walikuwa wachezaji 10 uwanjani, tuliweza kutumia mipira ya pembeni kuwatatiza na kuzidisha uvamizi. Ni vyema tulipata alama zote tatu,” akaongeza kocha huyo.

Arsenal ambao hawajacheza mechi moja ikilinganishwa na nambari tano Chelsea, watakuwa nyumbani dhidi ya Crystal Palace kwenye mechi ya EPL Jumapili Aprili 21.