Makala

EMILY ACHIENG': Nilitaka kuwa mtawa lakini nikatumbukia kwa mawimbi ya uigizaji

August 12th, 2019 2 min read

Na JOHN KIMWERE

SURA na jina lake siyo geni kwa wapenzi wa tasnia ya uigizaji hapa nchini. Anaodhoroshwa kati ya wasanii wa kike wanaovumisha ulingo wa burudani ya maigizo huku wakilenga kutinga upeo wa juu miaka ijayo.

Hakika ni mrembo mwenye tabasamu ya kuvutia ambaye ametunukiwa sauti nzito kama mwanaume.

Hayo tisa. Kumi, tangu utotoni mwake Emily Elizabeth Achieng alidhamiria kuwa mtawa lakini hakutarajia wala hangeweza kuamini kuwa angeibuka mwigizaji. Hata hivyo anasema kifo cha mamake mzazi takribani miaka 19 iliyopita kiliyeyusha ndoto yake kuwa mtawa.

Katika mpango mzima anajivunia kushiriki miongoni mwa vipindi maarufu hapa nchini kama: Papa Shirandula na Inspekta Mwala ambazo hupeperushwa kupitia Citizen TV. Katika uhusika wake anafahamika kwa majina mbali mbali ikiwamo ‘Cotney’ na ‘Yegon’s Wife’ kati ya mengine.

Ukistaabu ya musa utayaona ya firauni. Mwaka 2010 alibahatika kumsindikisha dadake, Beatrice Akoth kushiriki majaribio ya uigizaji kwenye ukumbi wa Bomas of Kenya ambapo bosi wa kundi la KEN TV, Onesmus Muthuri alitambua kipaji chake baada ya kusikia sauti yake.

”Kusema kweli binafsi kujiunga na maigizo haikuwa mteremko maana ni wazo halijawahi kuwa katika akili yangu pia waliotambua kipaji chake walikuwa wakitumia lugha geni kwangu,” alisema na kuongeza kuwa safari yake katika uigizaji ilianza kama mzaha lakini leo hii anajivunia mengi.

Anadokeza kwamba kipindi hicho alikuwa akifanya kazi za suluhu hasa vibarua vya kuosha nguo kwenye mitaa ya Nairobi. Anasema kipindi hicho maisha yalikuwa magumu zaidi kwake.

Msanii Emily Elizabeth Achieng. Picha/ John Kimwere

Mwanzo wa ngoma alishiriki filamu ya ‘Nairobi Law’ kama polisi. Kwa jumla ameshiriki filamu nyingi tu ikiwamo Auntie Boss (NTV), Sue Jonny (Maisha Magic East TV), Tabasamu (Citizen TV), Double Trouble (Ebru TV) na Curse kati ya zinginezo. Kupitia filamu ya ‘Curse’ aliteuliwa kuwania tuzo kitengo cha ‘Best lead Actress 2017.’ Pia anaamini anayo nafasi nzuri kunasa tuzo katika sekta ya uigizaji.

”Kamwe siwezi kusahau mwaka 2014 ulikuwa mwema kwangu ambapo nilifanikiwa kushiriki kipindi cha ‘Santalal’- TV Series kilichopeperushwa kupitia Citizen TV. Kusema ukweli kipindi hicho kilinifungua macho pia kunipiga jeki pakubwa katika uigizaji wangu,” alisema na kuongeza kwamba kwake ilikuwa nafasi nzuri kuwa mhusika mkuu kwenye filamu za kipindi hicho.

Kadhalika anasema kuwa alibahatika kufanya kazi na waigizaji mahiri kwenye filamu za Kinigeria (Nollywood) akiwamo Michael Kayode na Desmond Eliot kati ya wengine.

Dada huyu anasema haachwi nyuma ambapo kwa wanaotamba duniani kwenye filamu za Hollywood angependa kumfikia pia kufanya kazi naye mzalendo mwenzake, Lupita Nyong’o na Benjamin Onyango.

Kwa wenzie wa Nollywood anatamani kushirikiana nao Chioma Akpota na Ngozi Ezeonu kati ya wengine. Hata hivyo hapa nyumbani anataka kufanya kazi na waigizaji kama Pretty Mutave na Team Pete.

Pia ameshiriki matangazo ya ‘Viusasa’ kwa lugha ya Dhaluo kwenye redio ya Ramogi FM inayomilikiwa na Royal Media Services(RMS). Kadhalika ameshiriki matangazo ya kuigiza sauti kwenye Redio Mayienga bila kusahau Mojo Production.

Anasema serikali inapaswa kuamini kazi za waigizaji wa humu nchini na kuwekeza katika sekta ya maigizo ili kusaidia wasanii chipukizi. Anasema sekta ya filamu imegubikwa na changamoto nyingi tu ikiwamo malipo duni kati ya zingine.