Habari Mseto

Emitik wakali wa nyimbo za kitamaduni tamashani

June 9th, 2019 1 min read

NA RICHARD MAOSI

Tamasha za muziki 2019 katika Kaunti ya Nakuru zilitamatika Jumamosi kwenye shule ya wavulana ya Utumishi Boys Academy Gilgil.

Tamasha hizo zilianza rasmi siku ya Alhamisi na kuhusisha shule za upili kwa wavulana na wasichana, kutoka kaunti ndogo 11 zinazozunguka Nakuru.

Akizungumza na Taifa Leo Dijitali, katibu wa Kaunti ya Nakuru anayesimamia tamasha za muziki, John Atuti alisema zaidi ya shule 160 zilishiriki.

“Wanafunzi 5000 kutoka kaunti ya Nakuru walijitokeza kuonyesha vipaji vyao katika sanaa za maigizo,michezo na mashairi,”Atuti akasema.

Atuti alisema kati ya majimbo 47 kote nchini, kaunti ya Nakuru imekuwa ikifanya vyema ya punde zaidi ikiwa ni nambari mbili kitaifa miaka miwili iliyopita.

Moses Orangi, mwanafunzi kutoka Shule ya Upili ya Wavulana ya Jomo Kenyatta akionyesha ujuzi wake kupiga ngoma za kitamaduni. Picha/ Richard Maosi

Tamasha za muziki mwaka huu zilikuwa na daraja zaidi ya 600, zikiwasilishwa katika lugha ya Kiswahili na Kiingereza.

Alieleza kuwa mada kuu zinaendana na ajenda nne za serikali ambazo serikali iliahidi kutimizia raia wake kabla ya 2022.

Katibu wa muziki eneo la Bonde la Ufa Moureen Kirwa alisema washiriki watatuzwa kulingana na kitengo wanachoshiriki.

Aidha aliwahakikishia wanafunzi kuwa alama zitatolewa kwa njia ya uwazi bila kuegemea upande wowote,muradi wazingatie kanuni zote za utunzi.

“‘Tunawahimiza wanafunzi kuzingatia tamaduni za mwafrika,bila kutukuza sana mambo ya kigeni,”aliongezea.

Aliwashauri wanafunzi kutumia ala za muziki ili kuongeza ladha katika mawasilisho yao kama vile ngoma na tarumbeta.

Wanafunzi wa Shule ya Upili ya Athenai, Kaunti ndogo ya Marigat wakishiriki kwenye tamasha za muziki 2019. Picha/Richard Maosi

Shule zilizofanya vyema ni Goshen Secred kutoka Lanet ,Kenyatta Secondary na Ngecho kwa kuwasilisha nyimbo kutoka Afrika Magharibi.

Shule ya Upili ya Emitik ilifanya vyema kwa kuwabwaga jumla ya wapinzani 12 walioshiriki katika kitengo cha nyimbo za utamaduni.

Emitik walijizolea jumla ya alama 84 na sasa watashiriki katika kiwango cha maeneo kuanzia tarehe 19 hadi 29 Juni.

Lalmudia walifanya vyema kwenye kitengo cha nyimbo kutoka jamii ya Maasai na Jemps.

Washindi wawili kutoka kila kitengo wamefuzu kushiriki katika kiwango cha maeneo katika shule ya upili ya Langalanga, Kaunti ya Nakuru.