Makala

EMMA SAMUEL: Si kazi rahisi kuwa 'video vixen'

November 22nd, 2019 2 min read

Na JOHN KIMWERE

MWANZO kila mja hujipa matumaini ambapo huwa ni hali ya kutarajia. Ni katika kutumainia na kuvumilia ambapo anaamini nyota yake itang’aa na kuibuka mwigizaji wa kimataifa.

Anasema ingawa ndio ameanza kucheza ngoma analenga kukuza talanta yake katika maigizo akipania kutinga upeo wa kimataifa miaka ijayo.

Katika mpango mzima Emma Samuel anasema anataka kendeleza taaluma ya maigizo akilenga kufikia hadhi ya waigizaji mahiri duniani kama Taraji Penda Henson maarufu Cookie aliye mzawa wa Marekani.

Mwigizaji huyo alijizolea sifa tele kutokana na filamu zake maarufu ikiwamo ‘Empire,’ ‘What men want,’ ‘Baby boy,’ na ‘Hidden figures’ kati ya zinginezo. Kichuna huyu kisanaa anafahamika kama Tecler pia Tee.

Binti huyu ni mwigizaji na video vixen ambapo kando na sanaa chipukizi huyu anasomea kuhitimu kwa shahada ya digrii katika masuala ya sayansi ya siasa na uhusiano mwema katika Chuo Kikuu cha Kisii kitivo cha Nairobi (Nairobi Town Campus).

“Ninaamini nina talanta katika masuala ya sanaa maana kama video vixen ndani ya mwaka huu pekee nimefanikiwa kushiriki zaidi ya nyimbo 12 tofauti,” anasema na kuongeza hali hiyo imempa motisha zaidi katika sekta hiyo.

Kama video vixen chipukizi huyu mwenye umri wa miaka 19 anajivunia kushiriki nyimbo kama ‘Only you’ ‘Better release,’ ‘Bad Girl,’ na ‘Hot you,’ kati ya zinginezo.

”Kusema kweli naweza kusema nazidi kubobea kama video vixen maana nilianza kucheza densi tangu nikiwa mdogo. Ingawa nimekuwa nikipokea malipo kiasi nafasi nilizopata zimenijenga pakubwa katika sekta ya burudani,” alisema.

Emma Samuel. Picha/ John Kimwere

Katika maigizo kipusa huyu anajivunia kushiriki filamu mbili ikiwamo ‘Hallo Mr Right’ na ‘Empress’ ambazo zimepata mpenyo na kupeperushwa kupitia Rembo TV na Maisha Maigic mtawalia.

Kadhalika ameshiriki filamu fupi iitwayo ‘Zuri’ iliyotengenzwa na kundi la Machawook inayoonyeshwa kupitia mtandao wa Youtube.

Pia ameshiriki komedi inayokwenda kwa jina ‘Madhara ya noti mpya ya Kenya’ pia inayoonyeshwa kupitia Youtube. Komedi hiyo imetengenzwa na Mbuzi Seller Production.

”Katika uigizaji binafsi nalenga kujibiidisha kuhakikisha ninafaulu kushiriki filamu kama mhusika mkuu ili kujijenga zaidi katika maigizo pia kuvuna vinono,” alisema.

Kisura huyu anasema wanawake wanaoshiriki uigizaji hupitia pandashuka sio haba. Anadai nyakati zingine hukosa kulipwa licha ya kufanya kazi hali ambayo hufanya baadhi yao kuvunjika moyo na kuwazia kusepa.

”Kando na hayo nimejikuta kwenye wakati mgumu maana maprodyuza wengine hupenda kunishusha hadhi na kuniomba tuwe wapenzi ili kunipa ajira,” anasema na kuongeza kuwa suala hilo limemfanya anyimwe kazi takribani mara tano.

Anakiri kwamba ukosefu wa soko hutatiza tasnia ya uigizaji nchini. Kipusa huyu anashauri wenzake watie bidii wala wasivunjika moyo wanaposaka ajira ya uigizaji pia wamwaminie Mungu.