Habari

#EndLecturersStrike: Kero mitandaoni wanachuo wakimsihi Uhuru asuluhishe mgomo

April 30th, 2018 2 min read

Na PETER MBURU

WANAFUNZI wa vyuo vikuu vya umma nchini wametumia mitandao ya kijamii kuonyesha ghadhabu zao, wakinuia kumfikishia Rais Uhuru Kenyatta ujumbe namna walivyoathirika kielimu na kumtaka asuluhishe mgomo huo.

Wanafunzi hao walifanya hamasisho la saa moja wikendi, kwa posti za Twitter wakiwajumuisha Rais, Waziri wa Elimu na mashirika ya habari kama mbinu ya kupasha taifa habari za adhari wanazopata kutokana na mgomo huo.

Hamasisho hilo lenye hashtegi #EndLecturersStrike na #OkoaUniversity  liliwataka wanafunzi kuchangia zaidi ya posti milioni moja zikieleza mahangaiko ya wanafunzi kufuatia mgomo huo.

Kila mwanafunzi alihitajika kutuma posti 20 na kuwahusisha Rais, Waziri wa Elimu Amina Mohamed na angalau mashirika makuu ya habari nchini.

Wakati wa zoezi hilo, maelfu ya wanafunzi walieleza namna wanavyoathirika, huku wakimtaka Rais mwenyewe kuingilia kati na kuwaokoa, wakisema masomo katika taasisi za juu za elimu yamedorora kwa viwango vikubwa.

Wanafunzi walisema waziwazi kuwa serikali ilikuwa ikijikokota sana kusuluhisha tatizo hilo sugu, wakitaka taifa kulitambua kama janga la kitaifa katika kampeni hiyo iliyodumu kati ya saa sita na saa saba mchana wa Jumapili.

“#okoaUniversity @UKenyatta mimi pamoja na wanafunzi wenzangu 600,000 tumechoka. Tunarudi darasani lini? Maliza mgomo wa wahadhiri #LecturersStrikeKE,” akaandika @connienyakio.

“#EndLecturersStrike wanasiasa ambao wana wao wanasomea vyuo kama Havard, Cambridge, Yale na Leeds hawatatishwa hata mgomo ukidumu miezi 20,” @IamNjokiKelvin.

“Tunamsihi Mheshimiwa Rais @UKenyatta na @AMB_A_Mohammed kumaliza mgomo wa wahadhiri. Wanafunzi wamechoshwa kabisa. Malizeni mgomo @KTNNews @citizentvkenya @RailaOdinga @WilliamsRuto @UASU_KE #EndLecturersStrike.”

Baadhi ya wanafunzi walieleza matatizo ya kifedha wanayopitia, haswa wanaoishi nje ya vyuo na ambao watalazimika kulipia kodi maradufu kutokana na muda uliopotea wakati wa mgomo.

“#EndLecturersStrike Kwa kawaida ninalipa Sh30,000 za makazi kwa kipingi cha mwaka wa masomo, sasa itanibidi kulipa Sh60,000 kwani mgomo umerefusha muda wa masomo, kwani nitalipa karo ama kodi.”

“@AMB_A_Mohammed tupeni ishara kuwa tutahudhuria madarasa. Mgomo wa wahadhiri sasa utajwe janga la kitaifa #okoauniversity.”

“#EndLecturersStrike @UKenyatta Ni wakati wako kuingilia kati sasa na kutoa suluhu ya kudumu kwa suala la mgomo wa wahadhiri. Kwa miaka mitatu iliyopita, wanafunzi wa vyuo vikuu hawajahudhuria masomo ifaavyo. Hii imewagharimu muda na pesa. @KTNNews @citizentvkenya.”

Wanafunzi hao walishikilia kuwa wataendelea na msukumo huo hadi Rais mwenyewe awape sikio na kushughulikia kilio chao.