Habari

Eneobunge la Thika latambulika kutumia NG-CDF kwa uwazi

November 12th, 2019 1 min read

Na LAWRENCE ONGARO

ENEOBUNGE la Thika limetangazwa rasmi na kujinyakulia tuzo ya matumizi bora ya fedha katika maendeleo za kutoka mfuko wa fedha za Hazina ya Ustawi wa Maeneobunge – National Goverment Constituency Development Fund – (NG-CDF).

Kamati ya kutathmini matumizi ya fedha ya awamu ya 18 inayotambulika kama Financial Report FIRE, imetambua juhudi za eneo la Thika kutumia fedha hizo kwa njia inayoeleweka katika mwaka wa makadirio ya fedha 2018/19.

Hafla hiyo ya utambulizi ilifanyika mwishoni mwa wiki jana katika hoteli moja ya kifahari jijini Nairobi.

Tuzo hiyo ambayo ni ya kipee hutolewa kila mwaka ambapo katika hafla hiyo ilidhaminiwa na kampuni tofauti kama la Capital Narket Authority, Institute of Certified Public Accountancy of Kenya, Securities Exchange na Public Sector Accounts Standard Board of Kenya.

Wakati wa hafla hiyo, mbunge wa Thika Bw Patrick ‘Jungle’ Wainaina alipongeza hatua hiyo akisema ni heshima kwake kama mbunge na wakazi wote wa Thika anaowakilisha.

“Ninataja hatua hiyo kama mwongozo wangu wa kuendesha maswala ya CDF kwa namna ya kipekee bila kuingiza siasa yoyote. Maafisa walioajiriwa wanaendesha kazi hiyo kwa ujuzi wa kutosha na hutekeleza wajibu wao bila ukabila wowote,” alisema Bw Wainaina.

Alizidi kueleza ya kwamba mji wa Thika unakaliwa na makabila na watu wa tabaka mbalimbali na kwa hivyo kila mmoja hupewa fedha hizo bila ubaguzi.

Hatua hiyo imewapa motisha wakazi wa Thika wakisema wameridhika na tangazo hilo linaloonyesha kuwa kweli mbunge wao anatekeleza wajibu wake bila kuegemea upande wowote.