Habari

Enzi mpya Raila akigeuka mtetezi sugu wa Matiang'i

June 28th, 2019 1 min read

Na RUTH MBULA

KWA mara nyingine, kiongozi wa ODM Raila Odinga, amemtetea vikali Waziri wa Usalama Fred Matiang’i, akimtaja kama mfanyakazi mwenye bidii katika kazi yake.

Kinaya ni kwamba, wawili hao walikuwa mahasimu kabla na baada ya uchaguzi mkuu uliopita.

Ijumaa, Bw Odinga alisisitiza kuwa wanaomhusisha Dkt Matiang’i na sakata ya dhahabu feki, wanafanya hivyo kutimiza maslahi yao ya kibinafsi.

“Huyu kijana anajua kufanya kazi. Lakini kuna wengine ambao nia yao kuu ni kuchafua jina lake kwa kumhusisha na sakata ya dhahabu bandia,” Bw Odinga alisema katika eneo la Manga Isecha.

Bw Odinga alieleza kuwa, amemfahamu waziri huyo kwa muda mrefu na kwamba ni mchapa kazi mwadilifu.

Kiongozi huyo wa upinzani alikuwa akiongoea jana katika kata ya Manga Isecha, eneo bunge la Kitutu Chache Kaskazini, Kaunti ya Kisii wakati wa mazishi ya marehemu Samson Maina, kaka ya aliyekuwa mwenyekiti wa KANU na mfanyabiashara wa Nakuru, Geofrey Asanyo.

Mei 2019, Bw Odinga alivunja kimya chake kuhusu sakata hiyo ya dhahabu alipozuru eneo hilo hilo na kudai kuwa Waziri Matiang’i hana hatia na ni “msafi kama pamba”.

Mazishi

Wakati huo, alikuwa amehudhuria mazishi ya Dkt David Gilbert Ombati ambaye alikuwa daktari wa babake, Jaramogi Oginga Odinga.

Alisisitiza kuwa kanda ya sauti ambayo ilikuwa ikisambazwa mitandaoni haikuwa na Dkt Matiang’i bali ilikuwa njama ya walaghai wenye nia ya kuharibu jina lake kwa manufaa yao.

Katika siku za hivi karibuni, Bw Odinga amekuwa akimtetea vikali waziri huyo hali inayoibua maswali kuhusu asili ya urafiki kati yao ikizingatiwa kuwa walikuwa mahasimu wakubwa kabla na baada ya uchaguzi mkuu wa 2017.

Wakati huo, Bw Odinga ambaye alikuwa mgombeaji urais kwa tiketi ya muungano wa upinzani (NASA), alimkashifu Dkt Matiang’i kwa kuamuru polisi kutumia nguvu kupita kiasi walipokuwa wakikabili maandamano ya wafuasi wake.