Michezo

EPL: Arteta amtia nari Aubameyang afunge mabao dhidi ya Leicester City

October 24th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

KOCHA Mikel Arteta ameshikilia kwamba fowadi na nahodha Pierre-Emerick Aubameyang atapania kutumia mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) itakayowakutanisha na Leicester City mnamo Oktoba 25 uwanjani Emirates kunyamazisha wakosoaji wake.

Aubameyang, 31, atajitosa ugani akiwinda bao la kwanza kutokana na mechi nne zilizopita ligini huku akipania pia kuendeleza ubabe uliomshuhudia akifunga bao la ushindi kwenye mechi ya Europa League iliyoshuhudia Arsenal wakiwapiga Rapid Vienna ya Austria 2-1 mnamo Oktoba 22.

Aubameyang amekuwa fowadi matata zaidi kambini mwa Arsenal tangu asajiliwe kutoka Borussia Dortmund ya Ujerumani mnamo Januari 2018.

Mbali na kutofunga mabao katika mechi nne zilizopita za EPL, kutong’aa kwake katika mechi kubwa za ligi dhidi ya Liverpool na Manchester City kulimweka katika ulazima wa kukosolewa na mashabiki.

Hata hivyo, sogora huyo anajivunia kufunga mabao 19 kutokana na mechi 29 zilizopita chini ya Arteta aliyepokezwa mikoba ya Arsenal mnamo Disemba 2019.

“Matarajio ya mashabiki ni kwamba Aubameyang lazima afunge bao katika kila mchuano kwa sababu ya ukubwa wa jina lake kwenye ulingo wa soka. Tuko hapa kumsaidia afaulu kufanya hivyo, kwa sababu ni jambo linalowezekana,” akatanguliza Arteta.

“Tutarajie kuona mambo makubwa dhidi ya Leicester. Ni matarajio ya kila mmoja kwamba Aubamenyang atapata nafasi nyingi za kuwa na mpira ndani ya kijianduku cha wapinzani na ushirikiano kati yake na viungo wanaostahili kumwandalia pasi za hakika utakuwa wa kiwango cha juu,” akaongeza sogora huyo wa zamani wa Everton na Arsenal.

Aubameyang amekuwa akiwajibishwa sana na Arteta pembezoni mwa uwanja, hatua iliyomshuhudia akitamba zaidi kwenye mechi za Kombe la FA dhidi ya Manchester City na Chelsea msimu uliopita wa 2019-20.