Michezo

EPL: Bao la Giroud dhidi ya Norwich City laisaidia Chelsea kukaa tisti katika nafasi ya tatu

July 15th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

KOCHA Frank Lampard amesema “anadai matokeo bora zaidi” kutoka kwa kikosi chake cha Chelsea kilichowafunga Norwich City 1-0 mnamo Julai 14, 2020 uwanjani Stamford Bridge.

Mfumaji wa zamani wa Arsenal, Olivier Giroud, 33, aliwafungia Chelsea bao hilo la pekee mwishoni mwa kipindi cha kwanza baada ya kushirikiana vilivyo na chipukizi Christian Pulisic, 21, na kumwacha hoi kipa Tim Krul.

Ushindi huo wa Chelsea uliwadumisha katika nambari ya tatu jedwalini na hivyo kuimarisha kabisa nafasi yao ya kumaliza kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu ndani ya mduara wa nne-bora.

Chelsea kwa sasa wanajivunia alama 63, nne zaidi kuliko Leicester City na Manchester United wanaofunga orodha ya tano-bora. Kesho itakuwa zamu ya Leicester waliotawazwa mabingwa wa EPL mnamo 2015-16 kuvaana na Sheffield United katika uwanja wao wa nyumbani wa King Power huku Man-United wakiwaendea Crystal Palace ugani Selhurst Park.

Kujikwaa kwa Man-United au Leicester katika mechi zao kutakuwa afueni kubwa kwa Lampard analenga kuwaongoza Chelsea kufuzu kwa soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) muhula ujao.

Nusura ushirikiano kati ya Giroud na Pulisic kwa mara nyingine katika kipindi cha pili karibu uwapE Chelsea bao la pili ila kombora la Pulisici ambaye ni mzawa wa Amerika, likapanguliwa na Krul aliyefanya kazi ya ziada.

“Katika kipindi kama hiki cha kampeni za msimu huu, muhimu zaidi ni matokeo mazuri yatakayotushuhudia tukitia kapuni alama tatu katika kila mechi bila ya kufungwa bao,” akatanguliza Lampard.

“Nahisi kwamba kikosi bado hakijafikia kiwango cha usakataji ninachokitaka, ila kwa sasa muhimu zaidi ni kuzoa alama zitakazotukweza pale tunapolenga kufika (nafasi ya nne jedwalini) mwishoni mwa msimu huu,” akaongeza kiungo huyo wa zamani wa Chelsea na timu ya taifa ya Uingereza.

Norwich waliokuwa wakishiriki mchuano huo baada ya kichapo cha 4-0 kutoka kwa West Ham United mnamo Julai 12 kuwashusha ngazi, walishindwa kabisa kuelekeza kombora lolote langoni pa Chelsea.

Kwa upande wao, Chelsea walijibwaga ugani wakitawaliwa na kiu ya kujinyanyua baada ya kupepetwa 3-0 na Sheffield katika mchuano wao wa awali wa EPL mnamo Julai 11 ugani Bramall Lane.

Chelsea kwa sasa wanajiandaa kuvaana na Man-United katika nusu-fainali ya Kombe la FA uwanjani Wembley mnamo Julai 19 kabla ya kuwaendea Liverpool ugani Anfield kwa kivumbi cha EPL mnamo Julai 22. Watafunga rasmi kampeni za EPL muhula huu dhidi ya Wolves mnamo Julai 26 uwanjani Stamford Bridge.

Norwich kwa upande wao wameratibiwa kuchuana na Burnley mnamo Julai 18 kabla ya kuaga rasmi kipute cha EPL msimu huu kwa kukabilia na Manchester City ugani Etihad.