Michezo

EPL: Fulham walaza West Brom na kujiondoka kwenye mduara hatari

November 3rd, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

FULHAM walisajili ushindi wao wa kwanza katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kwa kuwatandaika West Bromwich Albion 2-0 mnamo Novemba 2, 2020, uwanjani Craven Cottage.

Ushindi huo uliwaondoa West Brom ndani ya mduara unaojumuisha vikosi vilivyopo katika hatari ya kuteremshwa ngazi mwishoni mwa msimu huu.

Kikosi cha kocha Scott Parker kilijiweka kifua mbele kunako dakika ya 26 kupitia kwa Bobby Decordova-Reid kabla ya Ola aina kuongeza la pili dakika nne baadaye. Mabao yote ya Fulham yalichangiwa na kiungo Aleksandar Mitrovic.

Fulham nusura wafunge mabao mawili zaidi mwishoni mwa kipindi cha pili ila juhudi za Tom Cairney na Decordova-Reid zikazimwa na kipa wa West Brom.

Chini ya kocha Slaven Bilic, West Brom kwa sasa bado hawajasajili ushindi wowote ligini kutokana na mechi saba zilizopita na walishuka hadi nafasi ya 18 jedwalini kwa alama tatu, mbili pekee mbele ya Sheffield United na Burnley.

Mchuano huo uliokutanisha vikosi viwili vilivyopandishwa ngazi kushiriki kipute cha EPL mwishoni mwa msimu wa 2019-20, ulitawaliwa na wingi wa hisia.

West Brom walikamilisha kampeni za msimu jana za Ligi ya Daraja la Kwanza (Championship) nyuma ya Leeds United huku Fulham wakifuzu kwa EPL baada ya kuwazidi Brentford maarifa kwenye mchujo ulioandaliwa uwanjani Wembley, Uingereza.

Limbukeni hao wa EPL wamekabiliwa na mtihani mgumu ligini huku Fulham nao wakiokota alama moja pekee kutokana na mechi sita zilizopita.

Kwa upande wao, West Brom wamesajili sare mara tatu na kushuhudia chombo chao kikizamishwa mara tatu.

Fulham kwa sasa hawajashindwa na West Brom katika mechi 10 zilizopita ligini. Fulham wanajivunia kusajili ushindi mara nne na kuambulia sare mara sita tangu wapokezwe kichapo cha 2-1 katika EPL mnamo Oktoba 2010.

Kwa upande wao, West Brom hawajawahi kushinda mechi yoyote ugenini dhidi ya Fulham tangu Oktoba 1967. Wamesajili sare mara saba na kupoteza mara 10 kutokana na michuano 17 ya tangu wakati huo.

Fulham kwa sasa wanajiandaa kuvaana na West Ham United katika gozi la London mnamo Novemba 7 huku West Brom wakiwaalika Tottenham Hotspur mnamo Novemba 8, 2020.